1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Sri Lanka bado yakabiliwa na mkwamo wa kisiasa

Sylvia Mwehozi
11 Julai 2022

Hali ya kisiasa nchini Sri Lanka bado ni tete wakati viongozi wa upinzani wakishindwa kukubaliana juu ya nani atajaza nafasi zilizoachwa wazi na viongozi huku waandamanaji wakiendelea kupiga kambi Ikulu.

https://p.dw.com/p/4DwyS
Sri Lanka's Präsident Gotabaya Rajapaksa
Picha: Andy Buchanan/AP/picture alliance

Waandamaji wameendelea kusalia katika makaazi ya rais wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa siku ya Jumatatu, sambamba na ofisi yake iliyoko kando ya bahari, pamoja na makaazi ya waziri mkuu ambayo walivamia mwishoni mwa juma wakiwataka viongozi hao wawili kujiuzulu. Waandamanaji hao ambao ni kutoka kila kada ya maisha, wameapa kuendelea na upinzani wao hadi viongozi watakapojiuzulu rasmi.Rais na Waziri Mkuu Sri Lanka wajiuzulu baada ya maandamano

Hadi siku ya Jumapili, waandamanaji walikuwa wamekaa kwa usiku wa pili katika makazi ya rais, wakicheza muziki na kutumia vifaa vya ndani ikiwemo bwawa la kuogelea bila juhudi zozote za maafisa wa usalama kuwadhibiti katika majengo hayo matatu. Shabeer Mohammad ni miongoni mwa waratibu wa maandamano. "Huwezi kuwaamini. Tangu uhuru, tangu mwaka 48, tuliwaamini wanasiasa na tumepoteza kila kitu tulichokuwa nacho. Kwahiyo hatutowaamini tena. Tutasalia hapa hadi watakapojiuzulu."

Sri Lanka | Proteste gegen die Regierung
Waandamanaji katika bwawa la kuogelea la IkuluPicha: AFP

Rais Rajapaksa, amewasiliana rasmi na waziri mkuu Ranil Wickremesinghe siku ya Jumatatu juu ya azma yake ya kujiuzulu lakini waandamanaji wanamtaka aondoke haraka inavyowezekana. Naye waziri mkuu Wickremesinghe alisema mwishoni mwa juma kwamba yuko tayari kuachia ngazi lakini hadi pale serikali mpya itakapoundwa. Saa chache baadae spika wa bunge alidai kwamba rais Rajapaksa ataachia madaraka siku ya Jumatano, taarifa zilizothibitishwa na ofisi ya waziri mkuu.

Mzozo huo wa kisiasa umezidi kufukuta Jumatatu baada ya kundi la mawaziri tisa wa serikali kutangaza kwamba wataondoka mara moja ili kupisha njia kwa ajili ya serikali ya vyama vyote. Lakini kundi jingine la mawaziri lililokutana na waziri mkuu limeamua kusalia mamlakani hadi  uwepo wa serikali mpya.

Rais Rajapaksa hajaonekana au kusikika hadharani tangu Jumamosi na hajulikani alipo, ingawa ofisi yake ilisema jana Jumapili kwamba ameamuru usambazaji wa gesi ya kupikia na hivyo kuashiria kwamba bado yuko kazini. Viongozi wa upinzani wamo katika mazungumzo ya kuunda serikali mbadala ya Umoja, ikiwa ni sharti la haraka la taifa hilo lililoko katika ukingo wa kufilisika kuendelea na mazungumzo na shirika la fedha ulimwenguni kwa ajili ya mpango wa kulinusuru.

Kama vyama vya upinzani vitashindwa kuunda serikali hadi wakati Rajapaksa anajiuzulu, basi waziri mkuu atakuwa rais wa muda kwa mujibu wa katiba. Lakini kutokana na shinikizo la waandamanaji, upinzani unakusudia kutomruhusu kuchukua wadhifa huo kwa muda.

Maandamano nchini Sri Lanka yamekuwa yakiongezeka kwa miezi mitatu iliyopita juu ya uhaba mkubwa ya mafuta, dawa na chakula.