1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Rais na Waziri Mkuu Sri Lanka wajiuzulu baada ya maandamano

10 Julai 2022

Rais na Waziri Mkuu wa Sri Lanka wamekubali kujiuzulu baada ya kutokea kwa maandamano ya vurugu, baada ya nchi hiyo kutumbukia kwenye mzozo mkubwa wa uchumi.

https://p.dw.com/p/4DuU9
Präsident von Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa
Picha: Pradeep Dambarage/ZUMA Wire/dpa/picture alliance

Rais na Waziri Mkuu wa Sri Lanka wamekubali kujiuzulu baada ya kutokea kwa maandamano ya vurugu, wakati waandamanaji walipovamia makaazi ya viongozi hao wawili na kuchoma ofisi ya waziri mkuu kwa hasira baada ya nchi hiyo kutumbukia kwenye mzozo mkubwa wa uchumi.

Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe amesema ataachia ngazi mara tu baada ya serikali mpya kuingia madarakani, na saa chache baadaye spika wa bunge akasema Rais Gotabaya Rajapaksa amekubali kujiuzulu pia.

Soma pia: Polisi Sri Lanka yaamrishwa kuwafyatulia risasi waandamanaji

Shinikizo zilizidi kuongezeka kwa viongozi hao wawili baada ya mdororo wa kiuchumi kusababisha uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu, na kuwaacha watu wakihangaika kununua chakula, mafuta na mahitaji mengine.

Polisi yajaribu kuzima maandamano kwa kutumia gesi ya kutoa machozi

Sri Lanka | Proteste gegen die Regierung
Polisi wakikabiliana na waandamanaji waliokuwa wanalalamikia kudorora kwa uchumiPicha: Amitha Thennakoon/AP Photo/picture alliance

Polisi ya Sri Lanka ilijaribu kuzuia maandamano hayo kwa kutoa amri ya watu kutotoka nje, na baadaye kuiondoa amri hiyo baada ya wanasheria na wanasiasa wa upinzani kuikosoa amri hiyo na kuitaja kuwa kinyume cha sheria.

Mamia kwa maelfu ya waandamanaji walimiminika katika mji mkuu Colombo na kuyavamia makaazi ya Rajapaksa.

Soma pia: Waislamu Sri Lanka watakiwa kusali ibada ya Ijumaa majumbani

Picha za video zimeonyesha umati mkubwa wa watu wakisherehekea ndani ya kidimbwi cha kuogelea, huku wengine wakilala kwenye vitanda na kujipiga picha. Baadhi ya watu walipika chai, huku wengine wakitoa tangazo kutoka chumba cha mikutano wakiwataka rais na waziri mkuu kuondoka.

Haikuwa wazi iwapo Rajapaksa mwenyewe alikuwepo wakati huo, na msemaji wa serikali Mohan Samaranayake alisema hana taarifa yoyote juu ya aliko rais huyo.

Waandamanaji wavamia maakazi ya Rais na Waziri Mkuu

Sri Lanka | Proteste gegen die Regierung
Waandamanaji wakiogelea baada ya kuvamia maakazi ya raisPicha: AFP

Waandamanaji baadaye waliingia katika makaazi ya kibinafsi ya waziri mkuu na kuyachoma moto, ofisi ya Wickremesinghe imesema. Haikubainika mara moja iwapo waziri mkuu huyo alikuwepo ndani wakati uvamizi huo ulipotokea.

Awali, maafisa wa polisi waliwarushia gesi ya kutoa machozi waandamanaji waliokuwa wamekusanyika katika maakazi ya rais, wakipeperusha bendera na kuimba nyimbo. Kwa ujumla, zaidi ya watu 30 walijeruhiwa katika vurugu za jana Jumamosi.

Soma pia:Sri Lanka yatangaza hali ya dharura, idadi ya waliokufa yafika 290

Spika wa bunge Mahinda Yapa Abeywardena alisema katika taarifa yake kwa njia ya televisheni kwamba alimfahamisha Rajapaksa kwamba viongozi wa bunge walikutana na kuamua kuwa anafaa kuondoka madarakani, na kwamba rais alikubali ombi lao.

Hata hivyo, Rajapaksa atasalia madarakani kwa muda kuhakikisha makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani, Abeywardena aliongeza.

"Aliniomba niwafahamishe wananchi kwamba atajiuzullu Jumatano ya tarehe 13, kwa sababu kuna haja ya makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani,'' Abeywardena amesema.

Mbunge wa upinzani Rauff Hakeem amesema makubaliano yalifikiwa kwa spika wa bunge kukaimu nafasi ya rais.