1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Spika wa Tanzania asema matukio ya mauaji yasitangazwe

Deo Kaji Makomba
15 Septemba 2022

Nchini Tanzania, mjadala umeibuka kufuatia Spika wa bunge la nchi hiyo Tulia Ackson kushauri matukio ya mauaji ambayo yamekuwa yakitokea nchini humo yasitangazwe kwani kwa kufanya hivyo yanazidi kuchochea mauji mengine.

https://p.dw.com/p/4Gvx3
Tansania Dr. Tulia Ackson
Picha: Ericky Boniphace

Spika Tulia Ackson amehoji kuwa jeshi la polisi linapaswa kuangalia namna nyingine ya utoaji wa taarifa kuhusu vyanzo vya matukio hayo ya mauaji kwa vyombo vya habari. 

Kauli hiyo  imejiri huku kukiwepo na mfululizo wa matukio ya mauaji  yanayofanywa na baadhi ya watu nchini humu huku jeshi la polisi likitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa chanzo cha matukio hayo ni wivu wa kimapenzi na masuala ya imani za kishirikina.

Akizungumza katika mkutano wa Nane wa bunge la Tanzania, katika vikao vya bunge hilo linaloendelea mjini Dodoma, Spika Tulia amesema kuwa pamoja na hatua zinazochukuliwa na jeshi la polisi nchini Tanzania, lakini bado matukio ya mauaji yanaendelea kuongezeka nchini humo.

Tanzania yaanzisha operesheni dhidi ya ongezeko la mauaji

Aidha Spika Ackson ameenda mbali zaidi kwa kulitaka jeshi la polisi nchini humu, kueleza sababu zingine za chanzo cha matukio hayo ya mauji na sio sababu hizo za wivu wa kimapaenzi huku aikisema kuwa sababu hizo zinazokuwa zikitolewa na jeshi la polisi zinaweza kuwa ni kichocheo cha matukio hayo ya mauaji.

Hata hivyo kauli hiyo ya Spika wa bunge la Tanzania Tulia Ackson, imezua mjadala mkubwa nchini humu, huku ikiwaibua watu mbalimbali wakiwemo wadau wa masuala ya habari.

Tanzania: Visa vya mauaji na watu wasiojulikana katika eneo la Matevesi mkoani Arusha

Akizungumza na Idhaa hii, mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri nchini Tanzania, Deodatus Balile, amesema kuwa endapo mamlaka husika zikianza kuficha taarifa za mauaji mwishoe nchi itaelekea kubaya na kuongeza kuwa.

Katika siku za hivi karibu kumekuwa kukiripotiwa kutokea kwa matukio ya mauaji katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, huku jeshi la polisi nchini humu likeleza chanzo cha matukio hayo ya kikatili ni wivu wa kimapenzi na imani za kishirikina.