1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Visa vya mauaji mkoani Arusha

1 Februari 2021

Watu wamekuwa wakiuawa na watu wasiojulikana katika eneo la Matevesi, Arusha. Siku ya jumamosi wanawake waliandamana kupinga kuzikwa mwili wa mwanamke aliyeuawa na kushinikiza polisi kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

https://p.dw.com/p/3ofMJ
Archivbild Demonstration in Durban UN Klimakonferenz
Picha: Getty Images/AFP/A. Joe

Katika Kata ya Matevesi wilayani Arumeru mkoani Arusha, kina mama waliingia barabarani kuzuia zoezi la mazishi ya mwili wa mwanamke aliyefahamika kwa jina la Anna Ngida mwenye umri wa miaka 44 ambaye aliuwawa na watu wasiojulikana na mwili wake kukutwa barabarani ukiwa uchi wa mnyama. Kina mama hawa wanashinikiza jeshi la polisi kutoa majibu kwa haraka kuhusiana na matukio ya mauaji yanayoendelea huku wanaofanya vitendo hivyo wakiwa hawajulikani.

Kwa mujibu wa mashuhuda na wakazi wa kata ya Matevesi, watu wanaouwawa zaidi ni wanawake huku matukio hayo yakiendelea kuleta hofu ya nini hasa nia ya wauaji na kwanini hawakamatwi. Jeshi la polisi mkoani Arusha linasisitiza kuwa linaendelea kufanya uchunguzi wa matukio hayo na watu wanatakiwa kuondoa hofu na kushirikiana na jeshi hilo kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuwatia hatia watu wanaofanya vitendo hivyo.

Pamoja na serikali kuendelea kusisitiza kwamba wahalifu wanatoka miongoni mwa jamii, wananchi wanasema serikali haijalichukulia suala hili kwa uzito unaotakiwa.