1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SIPRI: Mauzo ya silaha yameongezeka duniani

Admin.WagnerD9 Desemba 2019

Ripoti mpya iliyotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Masuala ya Amani SIPRI imesema mauzo ya silaha duniani yamepanda kwa karibu asilimia 5 mwaka 2018 huku Marekani ikiwa kinara kwenye biashara hiyo.

https://p.dw.com/p/3US2U
Minigun Stand MG Symbolbild Waffenexporte
Picha: picture-alliance/dpa/J. Lo Scalzo

Katika ripoti ya SIPRI iliyochapishwa leo, mauzo ya kampuni kubwa 100 za utengezaji silaha duniani yamefikia dola bilioni 420 yakichangiwa pakubwa na manunuzi ya silaha yaliyofanywa na Marekani.

Nyongeza hiyo ambayo imepanda kwa asilimia 47 ikilinganishwa na viwango vya mauzo ya silaha vya mwaka 2002, inaashiria utengenezaji na uuazaji wa silaha duniani unapanda kwa kiwango cha juu ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002, wauzaji watano wakubwa wa silaha duniani ni kampuni za Marekani.

Wauzaji wa silaha nchini Marekani pekee wamedhibiti asilimia 59 ya thamani ya soko baada ya mauzo kufikia dola bilioni 246 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.2 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kampuni za Marekani zimenufaika na uamuzi wa utawala wa rais Donald Trump wa kufanya maboresho ndani ya majeshi yake ili kukabiliana na kitisho cha Urusi na China.

Lockheed bado kinara kwenye mauzo ya silaha

Südkorea und USA beginnen Luftwaffenübung NEU
Kampuni ya Lockheed hutengeneza ndege ya kivita chapa F-35 Picha: picture-alliance/dpa/YNA

Kampuni ya Marekani ya Lockheed Martin imeendelea kushika nafasi ya kwanza kwa kuongeza uuzaji na mauzo ya silaha ikiwakilisha asilimia 11 ya mauzo yote ya kampuni 100 za utengenezaji silaha duniani.

Mafanikio ya kampuni ya Lockheed yamechangiwa na mauzo ya ndege zake za kivita chapa F-35 kwa serikali ya Marekani na mataifa mengine.

Urusi imetajwa kuwa ya pili kwa uuzaji wa silaha ambapo mauzo yake yamefikia asilimia 8.6 ya thamani soko ikifuatiwa na Uingereza pamoja na Ufaransa.

Ripoti ya SIPRI haikuijumuisha China kutokana na kukosekana kwa takwimu za kutosha lakini utafiti wa taasisi unakadiria kuna kampuni tatu hadi za saba za kichina katika orodha ya kampuni 100 zinazozalisha silaha kwa wingi duniani.

SIPRI imesema kampuni mbili kubwa barani Ulaya za utengenezaji silaha za Airbus na MBDA nazo zimetanua uuzaji kutokana na mahitaji katika maeneo yaliyo na mizozo na mivutano duniani.

Kampuni za Uingereza zimesalia kuwa wazalishaji wakubwa wa silaha katika Ulaya magharibi zikiwa zimefanya mauzo yanayofikia dola bilioni 35.1 ingawa thamani hiyo ni anguko la asilimia 5 ikilinganishwa na miaka iliyotangulia.

Urusi nayo inapiga hatua kupitia kampuni zake 

Russland Moskau | S-400 Raketenabwehrsystem
Mfumo wa Urusi wa kuzuia makombora, chapa S-400Picha: Reuters/T. Makeyeva

Kampuni ya utengenezaji silaha nchini Urusi ya Almaz-Antei imeshika nafasi ya tisa kwa kujikingia dola bilioni 9.6 ambayo ni nyongeza ya asilimia 18 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Sehemu kubwa ya ongezeko hilo limechangiwa na mahitaji ya silaha ndani ya Urusi kwenyewe na mauzo kwa mataifa mengine hususan mfumo wake wa ulinzi wa makombora wa S-400.

Moja ya mnunuzi wa mfumo huo ni Uturuki, iliyo mwanachama wa jumuiya ya NATO ambayo iliendelea na mipango ya kupokea mfumo wa chapa S-400 wa Urusi licha ya kitisho kutoka Marekani.

Kulingana na ripoti ya SIPRI Arms mataifa mengine yaliyonufaika na mauzo ya silaha kwa wingi ni  Israel, India, South Korea, Japan, Turkey, Australia, Canada na Singapore.