1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Simu ya Rais Xi wa China kwa Zelensky ina tija gani?

1 Mei 2023

Rais wa China Xi Jinping aliwasiliana kwa mara ya kwanza kwa njia ya simu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy siku ya Jumatano. Je, mawasiliano hayo yana na tija gani katika mzozo huo?

https://p.dw.com/p/4Qkoy
Bildkombo Selenskyj und Xi Jinping
Picha: Ukrainian Presidentia/IMAGO/MONCLOA PALACE/REUTERS

Wakati wa mawasiliano hayo, China ilisisitiza kuwa msimamo wake thabiti ni kuhimiza mazungumzo ya amani huku ikiahidi kutuma mjumbe maalum nchini Ukraine na kufanya mazungumzo na pande zote zinazohusika katika mzozo huo unaoendelea.

Zelenskyy amebaini kuwa mazungumzo na Xi yalikuwa mapana na yenye tija. Ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa anaamini mawasiliano hayo, pamoja na uteuzi wa balozi wa Ukraine nchini China, vitasaidia katika msukumo wa kuboresha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Je, simu hiyo itabadili msimamo wa China?

Mawasiliano hayo ya simu ambayo ni ya kwanza kufahamika kati ya Xi na Zelenskyy tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi, yalipongezwa na Marekani, Umoja wa Ulaya, Ufaransa na Ujerumani huku Urusi ikisema inakaribisha hatua yoyote ambayo inaweza kusaidia kumaliza mzozo huo hivi karibuni.

Hata hivyo, Kremlin imesema bado inahitaji kufikia kwanza malengo yake katika kile wanachokiita "operesheni maalum ya kijeshi" nchini Ukraine. Ikulu ya White House imesema ni mapema mno kubaini iwapo mawasiliano hayo yanaweza kupelekea kufikiwa makubaliano ya amani kati ya Urusi na Ukraine.

Soma pia: Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andriy Melnyk amesema mchango wa China waweza kuwa halisi

Baadhi ya wataalam wanaunga mkono msimamo huo wenye tahadhari wa Washington wakisema mawasiliano hayo ya simu kati ya Xi na Zelenskyy hayaleti matumaini yoyote kuhusu msimamo wa China kunako mzozo huo.

Wu Qiang, mchambuzi huru mjini Beijing amesema simu ya Xi kwa Zelensky iligubikwa na mazungumzo yanayohusu urafiki kati ya China na Ukraine, na haikuweza kutoa mapendekezo madhubuti ya amani kwa mzozo unaoendelea na pia haikulaani uvamizi wa Urusi. Qiang ameongeza kuwa misimamo yote ya kisiasa ya China iliyotolewa kupitia mawasiliano hayo haikubadilika.

'Kutuliza hisia baada ya kauli tata'

Lu Shaye - Chinas Botschafter zu Frankreich
Lu Shaye, Balozi wa China nchini UfaransaPicha: MARTIN BUREAU/AFP/Getty Images

Wataalamu wengine wa masuala ya siasa wanasema China inataka kuendelea kujinadi kama "mpatanishi" kupitia mawasiliano ya simu ya Xi na Zelenskyy huku ikijaribu kutuliza hisia baada ya kauli tata iliyotolewa na Lu Shaye, balozi wa China nchini Ufaransa wiki hii.

Wakati wa mahojiano na shirika la utangazaji la Ufaransa TF1 , Lu alitilia shaka uhuru kamili wa nchi zilizokuwa zamani katika umoja wa Soviet, akidai kuwa hazina "hadhi kamili " chini ya sheria za kimataifa.

Ian Chong, Mtaalamu wa masuala ya siasa katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Singapore amesema matamshi ya Lu yaliwakwaza watu wengi barani Ulaya, jambo ambalo limepelekea China kuonesha juhudi za kumuunga mkono Zelenskyy kama jaribio la kuonyesha kuwa China inachukulia kwa uzito wasiwasi wa mataifa ya Ulaya juu ya masuala ya uhuru na amani.

Soma pia: China yataka mazungumzo ya amani yafanyike kati ya Urusi na Ukraine

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasema mawasiliano hayo kati ya Xi na Zelensky yanalenga zaidi ya kudhibiti uharibifu uliosababishwa na maoni ya Balozi Lu, kwani Beijing inatarajia kutumia mzozo unaoendelea wa Ukraine kujinadi kama taifa lenye nguvu kimataifa lenye uwezo wa kufanikisha mchakato wa amani.

Die Fahnen von China und der Ukraine nebeneinander
Bendera ya China na UkrainePicha: Viacheslav Chernobrovin/Zoonar/picture alliance

Zsuzsa Anna Ferenczy, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Dong Hwa nchini Taiwan anasema ilikuwa ni fursa ya kuonyesha taswira kwa wakazi wake kwamba kimataifa, China ni muhimu sana na inaweza kuendesha mchakato kama huo.

Bado kuna mashaka dhidi ya China

Wakati China ikiendelea kudhihirisha msimamo wake wa kutoegemea upande wowote katika vita vya Ukraine, wachambuzi na baadhi ya viongozi wa mataifa kadhaa ulimwenguni bado wana mashaka juu ya nia halisi ya Beijing.

Katika mahojiano ya kipekee na DW,  Rais wa Lithuania Gitanas Nauseda ametilia shaka uthabiti wa China kama mpatanishi, akisisitiza kwamba kitendo cha kulaani uvamizi wa Urusi kinapaswa kuwa sharti kuu kwa Beijing kabla ya kuwa mpatanishi wa kweli. Tangu Februari mwaka jana, China imekuwa ikiimarisha ushirikiano wake katika nyanja nyingi na Urusi.