1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za Qatar zawapiga marufuku abiria kutoka Afrika Kusini

Zainab Aziz Mhariri:Chilumba Rashid
27 Novemba 2021

Shirika la ndege la Qatar limesema kuanzia Jumamosi wasafiri kutoka Afrika Kusini, Zimbabwe na Msumbijihawataruhusiwa kutumia ndege zake.

https://p.dw.com/p/43ZSW
Katar Doha - Qatar Airline Landet
Picha: Getty Images/AFP/K. Jaafar

Kila muda unavyosonga mbele nchi zaidi zinaendelea kuziwekea marufuku ya usafiri nchi za kusini mwa Afrika huku ulimwengu ukitumbukia kwenye sintofahamu kutokana na kuzuka kwa virusi vipya corona aina ya Omicron ambavyo vinadhaniwa kuwa na uwezo wa kuwa sugu dhidi chanjo zinazotolewa sasa.

Nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Australia, Brazil, Canada, Iran, Japan, Thailand na Marekani, zimejiunga na nchi nyingine pamoja na nchi za Umoja wa Ulaya na Uingereza katika kuziwekea vikwazo nchi hizo za kusini mwa Afrika kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi hivyo vipya. Hata hivyo nchi hizo zimeweka vikwazo hivyo kinyume na ushauri uliotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linalosema hatua zinazochukuliwa na mataifa hayo zimechukuliwa haraka mno.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus Picha: Denis Balibouse/AP/picture alliance

Licha ya hatua kali za kuzuia safari za ndege, kuna ushahidi unaonyesha kuwa watu wanaoambukizwa virusi hivyo vipya wanaongezeka. Baadhi ya wasafiri katika nchi za Ubelgiji, Israel, Hong Kong, na Ujerumani tayari wamethibitishwa kuwa wameambukizwa virusi vipya vya corona. Mamlaka nchini Uholanzi inafuatilia hali kwa karibu baada ya abiria 61 kutoka kwenye ndege mbili zilizotokea Afrika Kusini kuthibitishwa kuwa waameambukizwa aina hiyo mpya ya ugonjwa wa kutwa COVID-19.

Waziri wa masuala ya kijamii katika jimbo la magharibi la Hesse, nchini Ujerumani, Kai Klose amesema wizara ya afya imethibitisha mtu wa kwanza aliyeambukizwa virusi hivyo vipya baada ya mtu huyo kurejea kutoka Afrika Kusini. Abiria huyo alishukia kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Frankfurt.

Waziri wa masuala ya kijamii wa jimbo la Hess, magharibi mwa Ujerumani,
Waziri wa masuala ya kijamii wa jimbo la Hess, magharibi mwa Ujerumani,Picha: Boris Roessler/dpa/picture alliance

Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO mnamo siku ya Ijumaa lilitangaza aina hiyo ya COVID-19 ya B.1.1.529 iliyogunduliwa hivi karibuni kuwa aina ya virusi vinavyotia wasiwasi, ambayo imepewa jina la Omicron.

Mamlaka ya afya ya Umoja wa Ulaya imesema kuwa aina hiyo mpya ya virusi inaelekea kuvuka kiwango cha hatari hadi kuwa kwenye kiwango cha kubwa sana kwa bara la Ulaya.

Maafisa wa Umoja wa Ulaya walikubaliana siku ya Ijumaa kuyahimiza mataifa yote 27 katika umoja huo kupiga marufuku safari kutoka mataifa kadhaa ya kusini mwa Afrika, sera ambayo Ujerumani tayari imeitekeleza.

Hofu juu ya uwezekano wa Ujerumani kurudi katika hatua karantini imewafanya viongozi wa biashara kutoa tamko. Ludwig Veltmann, anayeongoza chama cha wafanyabiashara wanaondesha biashara ndogo na za kati ameliambia shirika la Habari la Ujerumani Dpa kwamba vizuizi vyovyote vipya vitawaathiri maelfu ya wafanyakazi.

Kirusi kipya cha covid chapewa jina la Omicron
Kirusi kipya cha covid chapewa jina la OmicronPicha: Pavlo Gonchar/Zumapress/picture alliance

Ametoa wito wa kuhimizwa matumizi ya upimaji wa haraka ili kuepusha hatua za karantini, ili kufuatilia kwa karibu milipuko yoyote na kuweza kupambana nayo kulingana na misingi ya kikanda. Amesema hilo likifanyika maisha ya umma na uchumi hautaathiriwa nchini Ujerumani taifa lenye uchumi mkubwa inaloongoza kiuchumi uchumi mkubwa barani Ulaya.

Vyanzo:/DPA/AFP/RTRE