1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la haki za binaadamu lamtaka Bush kujitolea katika mzozo wa Darfur.

Mohammed Abdulrahman13 Februari 2006

Human rights Watch lasema Umoja wa mataifa upewe kibali cha kuwapokonya silaha Janjaweed.

https://p.dw.com/p/CHLh
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan akiwa na Rais wa Marekani George W.Bush
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan akiwa na Rais wa Marekani George W.BushPicha: AP

Shirika la haki za binaadamu Human rights watch, lenye makao yake makuu nchini Marekani, limesema Rais George Bush wa nchi hiyo hana budi kutoa msaada wa dharura ili harakati za umoja wa mataifa katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur ziweze kuwa na kibali na uwezo wa kuwalinda raia. Taarifa ya Shirika hilo imekuja katika wakati ambao Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan anakutana leo na Rais wa Marekani mji Washington .

Mkurugenzi wa Shirika hilo barani Afrika Peter Takirambudde alisema Rais Bush anawajibu wa kueleza wazi kwamba Marekani itatoa msaada wa dharura kwa ajili ya harakati za umoja wa mataifa katika jimbo la Darfur, na hana budi pia kuzitaka nchi nyengine kufanya hivyo. Pia Marekani inawajibu wa kushinikiza umoja wa mataifa uwe na kibali cha kuwapokonya silaha wanamgambo wa Janjaweed na kuwalinda raia, hata kama ni kutumia nguvu ikihitajika.

Atakapoelekea Washington leo kuonana na Rais George W. Bush wa Marekani, katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Anna anatarajiwa kutoa wito wa msaada mkubwa wa Marekani ili kuwalinda raia huko Darfur. Katika wadhifa wake kama Rais wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa mwezi huu kuanzia tarehe tatu Februari, Marekani ilitoa taarifa ikimtaka Bw Annan aanze kuandaa mpango wa harakati za umoja wa mataifa huko Darfur, ili kukabiliana na hali inayozidi kuwa mbaya katika jimbo hilo.

Wakati Shirika la human rights watch likitoa raia hiyo, mazungumzo ya amani ya Darfur yanaendelea katika mji mkuu wa Nigeria Abuja, chini ya upatanishi wa mjumbe maalum wa umoja wa Afrika Dr Salim Ahmed Salim. Mazungumzo hayo ya Darfur ambayo yamekabiliwa na mivutano ya mara kwa mara kati ya pande zinazohusika, sasa yamo katika duru yake ya Saba .

Lakini tangu mwishoni mwa mwaka jana, pande hizo zote zimeripotiwa kufanya mashambulio dhidi ya majeshi vya umoja wa Afrika na misafara ya misaada kwa raia, na hivyo kusababisha sehemu kubwa ya misaada hiyo kusitishwa kwa sababu ya hali mbaya ya usalama.

Mnamo mwezi ujao, wafadhili wanatazamiwa kukutana kuzungumzia mpango wa kugharimia zaidi harakati za kikosi cha kulinda amani cha umoja wa Afrika baada ya tarehe 31 Machi, pale muda wake utakapomalizika. Shughuli hizo zitahitaji msaada mkubwa wa fedha , mkakati na uungaji mkono ili kudumisha kipindi cha mpito hadi umoja wa mataifa utakapokua tayari kuchukua kikamilifu nafasi hiyo.