1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amadou Ba ateuliwa nafasi ya Waziri Mkuu wa Senegal

Zainab Aziz Mhariri:Tatu Karema
18 Septemba 2022

Rais wa Senegal Macky Sall amerejesha wadhifa wa Waziri Mkuu nchini mwake miezi miwili baada ya uchaguzi wa bunge uliokuwa na mivutano.

https://p.dw.com/p/4H1QN
Senegal I Amadou Ba
Picha: Andrew Caballero-Reynolds/REUTERS

Rais wa Senegal amemteua aliyekuwa waziri wa uchumi Amadou Ba katika wadhfa huo mpya ambaye pia ataliongoza baraza la mawaziri.

Rais wa Senegal Macky Sal
Rais wa Senegal Macky SalPicha: John Thys/AFP

Amadou Ba, mtaalamu wa masuala ya kodi mwenye umri wa miaka 61 amewahi pia kuwa waziri wa mambo ya nje wa Senegal.

Uteuzi wa Ba ambao umeifufua tena nafasi ya waziri mkuu katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi umefanywa baada ya wadhifa huo kuondolewa mnamo mwezi Aprili mwaka 2019.

Ba alisema kwenye televisheni ya taifa kwamba vipaumbele vikuu ambavyo rais Macky Sal ameviainisha ni pamoja na kuboreshahali ya uchumi kwa wananchi wa Senegal, kudhibiti mfumuko wa bei, usalama, makazi bora, mafunzo ya ufundi stadi, ajira na shughuli za ujasiriamali.

Rais Macky Sall amesema waziri mkuu huyo mpya atawajibika katika kushughulikia kupanda kwa gharama za maisha.

Uchaguzi wa Bunge nchini Senegal ambapo muungano wa Rais Macky Sal ulipoteza wingi wa viti bungeni.
Uchaguzi wa Bunge nchini Senegal ambapo muungano wa Rais Macky Sal ulipoteza wingi wa viti bungeni.Picha: Johan Wessels/AFP

Nafasi hiyo ya Waziri Mkuu imeanzishwa wakati Senegal inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi, ambayo kwa sehemu kubwa yanatokana na janga la COVID-19 na athari zinazoukumba ulimwengu kutokana na vita vya nchini Ukraine.

Wasiwasi juu ya utawala wa Rais Macky Sal unaendelea kujitokeza huku akituhumiwa kwa kutaka kuvunja ukomo wa mihula miwili uongozini hatua itakayomwezesha kugombea urais tena ifikapo mwaka 2024. 

Maandamano makubwa yalifanyika nchini Senegal mwaka jana wakati Ousmane Sonko, mpinzani mkuu wa Sall aliyeibuka wa tatu kwenye uchaguzi wa rais mwaka 2019 alipokamatwa kwa tuhuma za ubakaji ambapo amekanusha kuhusika.

Raia walioandamana kupinga kukamatwa kwa Ousmane Sonko
Raia walioandamana kupinga kukamatwa kwa Ousmane SonkoPicha: SEYLLOU/AFP/Getty Images

Kwenye uchaguzi wa bunge uliomalizika nchini Senegal, muungano unaotawala wa rais Macky Sall ulipoteza wingi wa viti bungeni.

Rais Macky Sall pia ametofautiana na mshirika muhimu kwenye kambi yake, waziri mkuu wa zamani Aminata Mimi Toure, ambaye hakuchaguliwa kuliongoza bunge la kitaifa na tangu wakati huo ameulaani utawala wa Sal kwa "ukosefu wa haki."

Vyanzo:RTRE/AFP