1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sama Lukonde Kyenge ateuliwa Waziri Mkuu mpya wa DRC

Jean-Noel Bamweze 16 Februari 2021

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Felix Tshisekedi amemteua mkuu wa shirika la madini kuwa waziri mkuu mpya, kufuatia mapambano ya muda mrefu ya kuwania madaraka na washirika wa mtangulizi wake Joseph Kabila.

https://p.dw.com/p/3pPux
Afrika  Premierminister der Demokratischen Republik Kongo,  Sama Lukonde Kyenge
Picha: Giscard Kusema

Waziri Mkuu mpya Jean-Michel Sama Lukonde Kyenge, amesema kipaumbele chake kitakuwa usalama na uthabiti katika taifa hilo linalozongwa na mizozo ya kivita.  

Jean-Michel Sama Lukonde Kyenge, mwenye umri wa miaka 43, ambaye uteuzi wake ulitangazwa katika amri ya rais iliyosomwa kwenye televisheni, anachukuwa nafasi ya Sylvestre Ilunga Ilukamba, aliyelazimishwa kujiuzulu baada ya muungano kati ya wafuasi wa Tshisekedi na rais wa zamani Kabila kuvunjika.

Sama Lukonde amewambia waandishi habari kwamba kurejesha hali ya usalama ndiyo kitakuwa mmoja ya vipaumbele vyake vya juu, hasa katika eneo la mashariki na Katanga, eneo la uchimbaji madini anakotokea.

"Usalama, kama munavyojua, ni moja ya vipaumbele, haswa mashariki mwa Kongo na huko Katanga. Pamoja na maswala ya usalama, tuna pia maswala ya kijamii, ile ya maendeleo, maswala ya kisheria na pia swala la elimu kwa wote. Tuligusia mengi kuhusu mageuzi kwani yanahitajika katika sekta kadhaa," alisema Lukonde.

Sylvestre Ilunga Ilunkamba | Ehemaliger kongolesischer Premierminister
Sylvestre Ilunga Ilunkamba waziri mkuu aliyejiuzuluPicha: Giscard Kusema

Taifa la Congo ambalo ndiyo kubwa zaidi katika kanda ya Afrika kusini mwa Sahara, lina sifa ya rushwa, utawala mbaya na ukosefu wa usawa. Eneo la mashariki mwa nchi linakabiliwa na vurugu zinazohusisha makundi ya silaha, likiwemo la ADF, ambapo watu zaidi ya 900 wameuawa au kutoweshwa katika nusu ya mwisho ya mwaka 2020 tu kulingana na Umoja wa Mataifa.

Wakati wa kampeni zake, rais Tshesekedi aliahidi kukabiliana na umaskini na rushwa, na pia kuboresha rekodi mbaya ya taifa hilo kuhusu haki za binadamu. Lakini miaka yake miwili ya kwanza madarakani iligubikwa na mtangulizi wake. Baadhi ya raia wameeleeza matumaini yao kwa waziri mkuu huyo mpya, kama François Mukendi, mhitimu kwa miaka lakini bado hana kazi.

"Nimekuwa sina ajira kwa muda mrefu. Sisi watu wasio na kazi tunafikiria kutakuwa na ajira. Maisha ya kijamii na utawala bora ndio tunatarajia".

Miaka miwili ya Tshisekedi, kuna yapi mapya?

Sama Lukonde, ambaye aliwahi kuwa waziri wa michezi chini ya Kabila, anatokea chama kidogo cha Mustakabali wa Congo (ACO), ambacho kiliwahi kushirikiana na tajiri wa Katanga Moise Katumbi, lakini kilimuunga mkono Tshisekedi katika uchaguzi wa 2018. Aliteuliwa na Tshisekedi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya taifa ya madini ya Gecamanine Juni 2019.

Lakini uteuzi wa waziri mkuu huyo mpya haujapokelewa vyema na kila mtu. Floribert Anzuluni, mratibu wa kampeni ya kiraia iitwayo Filimbi,  amesema uteuzi huo ni ishara ya kuhuishwa na tabaka la watawala nchini Congo.