1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiRwanda

Rwanda yaituhumu UNHCR kwa kudanganya kuhusu wahamiaji

13 Juni 2024

Serikali ya Rwanda imelituhumu Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kwamba lilidanganya kuwa waomba hifadhi wanaotarajiwa kupelekwa nchini humo huenda wakahamishwa tena.

https://p.dw.com/p/4gz51
Rwanda yakanusha shutuma za shirika la UNHCR kuhusu wahamiaji
Rwanda yakanusha shutuma za shirika la UNHCR kuhusu wahamiajiPicha: Tayfun Salci/ZUMA Press Wire/picture alliance

Rwanda imelituhumu Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa - UNHCR kwamba lilidanganya wakati lilipoieleza mahakama ya Uingereza mapema wiki hii kuwa waomba hifadhi wanaosubiri kupelekwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki huenda wakahamishwa tena katika nchi ambako wanaweza kukabiliwa na mateso na vifo.

Jumatatu wiki hii, mawakili wa UNHCR, walisema kuwa mfumo wa Rwanda wa waomba hifadhi hauna ufanisi, kama sehemu ya changamoto ya sera ya serikali ya Uingereza ya kuwahamisha waomba hifadhi na kuwapeleka Kigali.

Mawakili hao walidai kwamba sera hiyo inawaweka hatarini waomba hifadhi wanaokabiliwa na kitisho cha kurejeshwa kwenye nchi zao, hoja ambazo zilitumiwa na mahakama ya juu ya Uingereza wakati ilipotoa uamuzi mwaka jana kwamba mpango huo ulikuwa kinyume cha sheria.

Katika taarifa yake, serikali ya Rwanda imedai kwamba "UNHCR ilidanganya" na kwamba "shirika hilo linaonekana kuwa na dhamira ya kuwasilisha madai ya uongo katika mahakama za Uingereza juu ya namna Rwanda itakavyoashughulikia waomba hifadhi, wakati pia ikiendelea kushirikiana kuwaleta wahamiaji kutoka Libya kwa usalama nchini Rwanda".