1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robert Lewandowski awa mchezaji bora wa Ulaya

2 Oktoba 2020

Baada ya kutendewa isivyo kwenye tuzo ya Ballon d'Or, Robert Lewandowski ameshinda tuzo ya mtu mmoja ya soka ya Ulaya. Kocha wake Hansi Flick, pia ametambuliwa na UEFA.

https://p.dw.com/p/3jMIv
Schweiz | Fußball Champions League | Auszeichung Robert Lewandowski
Picha: UEFA Pool/Reuters

Mshambuliaji wa klabu ya Bayern Munich Robert Lewandowski ametajwa kuwa mchezaji bora wa kiume barani Ulaya kwa mwaka 2020 siku ya Ahamisi na shirikisho la Mpira wa Miguu barani Ulaya UEFA.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 32 kutoka Poland, alimpiku mchezaji mwenzake wa Bayern Manuel Neuer na kiungo wa kati wa Manchester City Kevin De Bruyne kushinda taji hilo.

Soma pia: Lewandowski achaguliwa mshambuliaji bora wa Bundesliga

Lewandowski alifunga magoli 55 katika michezo 47 msimu uliyopita wakati Bayern iliponyakuwa mataji matatu kwa kushinda Ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga, Kombe la Ujerumani na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya - Champions League. Hii ndiyo mara ya kwanza kwa Lewandowski kushinda tuzo ya UEFA.

Bundesliga Fussball - Bayern Munich vs. Schalke 04
Lewandowski aliifungia Bayern Munich magoli 55 msimu uliyopita.Picha: Michael Dalder/Reuters

"Nashukuru sana, najivunia sana na nina furaha sana," alisema Lewandowski. "Unapofanya kazi kwa bidii na kisha unapata zawadi hii, ni jambo maalumu sana."

Najivunia timu nzima kwa yale tuliyofanikisha," aliongeza.

Pernille Harder, Hansi Flick wapata tuzo

Kiungo wa mbele wa zamani wa Wolfsburg Pernille Harder, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Chelsea ya England, alishinda zawadi ya wanawake, huku kocha wa Lewandowski, Hansi Flick, akishinda tuzo ya kocha wa mwaka.

Soma pia:Lewandowski atangazwa mchezaji bora na jarida la Kicker

Lewandsowski alihamia Ujerumani kutoka Poland 2010 na alikuwa sehemu muhimu ya timu ya Borussia Dortmund chini ya kocha Jürgen Klopp. Alihamia Bayern Munich 2014 akitazamia kombe la Ulaya, ambalo hatimaye liliwasili Agosti baada ya Bayern kuishinda Paris Saint-Germain 1-0 katika fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Akiwa tayari na goli moja na kusaidia matano katika michezo minne, Lewandowski atatazamia kuendeleza harakati zake za kufunga magoli msimu huu. Atashiriki pia katika mashindano ya Bingwa wa Ulaya ya 2020 yalioahirishwa mwezi Juni 2021 kama nahodha wa timu ya taifa ya Poland.

Soma pia:Lewandowski ni moto wa kuotea mbali

Lewandowski alitendewa ndivyo sivyo mapema mwaka huu, wakati jarida la michezo la Ufaransa lilipotangaza kwamba halingetoa tuzo ya heshima ya Ballon d'Or msimu huu kutokana na janga la virusi vya corona. Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA, lilisema mwezi Septemba litaendelea na mipango ya kutoa tuzo za ubora za FIFA licha ya janga hilo.

Chanzo: AFPE, DPAE