1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RIPOTI YA MAZINGIRA 2003

Johannes Beck / Ahmed M. Saleh2 Januari 2004
https://p.dw.com/p/CHix
2003 ungeliweza kuwa mwaka wenye mwamko mkubwa zaidi wa kimazingira. Kiangazi cha joto kali kiliidhihirishia Ulaya ya Kati athari zinazoweza kutazamiwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa: Ukame, ukosefu wa mavuno na kufariki kwa watu elfu kadha. Lakini mwamko huo wa hifadhi ya mazingira umezidi kudhoofika miongoni mwa raiya. Hifadhi ya maumbile na ulinzi wa mali ya asili si miongoni mwa mambo yanayopewa umbele wakati huu, anasema mwandishi wetu Johannes Beck katika ripoti yake hii fupi ya Mazingira mwaka 2003. Matatizo ya kimazingira katika sehemu mbali mbali za dunia yanadhihirika zaidi katika sekta ya hifadhi ya hali ya hewa: Wakati, upande mmoja taratibu kinaendelea kuzama kisiwa cha Tavula katika Bahari ya Pasifiki, upande wa pili wa Pasifik, Marekani inaendelea kuzitumia nishati za dunia kwa isirafu kubwa. Wala athari zake hazina umuhimu wowote kwa serikali ya sasa ya Marekani inayotoa hoja kwamba hifadhi ya hali ya hewa inailetea gharama kubwa mno. Mtindo wa kuishi Kimarekani, yaani "American Way of Life", maisha ya kutumia kwa isirafu petroli katika magari yao ya anasa, kuwa na makarakana makukuu mno yanayotumia kupita mpaka nishati ya makaa pamoja na nyumba za familia zinazotumia mafuta mengi ya kupashia moto kwa sababu hazikujengewa kinga ya kutosha dhidi ya baridi. Kwa sababu hizo Marekani huungana na Urusi, dola kuu la pili, kuiwekea vizingiti Protokali ya Kyoto ya hifadhi ya hali ya hewa. Lakini nayo Ujerumani yenye kusifiwa kwa harakati zake nzuri za kifadhi ya mazingira, haikuwa na mwaka wa mafanikio. Japokuwa serikali na upinzani zimeweza kuwafikiana kuchukua hatua za mwamzo za marekibisho ya kiuchumi ili kupunguza matumizi ovyo, lakini zingeweza pia kushughulikia zaidi hifadhi ya mazingira. Kwa mfano mashirika ya ndege hupeleka madege yao makubwa kila sehemu ya dunia bila ya kulipa kodi ya kuchafua mazingira, wakati mashirika ya treni yenye kuhifadhi mazingira yanalipishwa kodi kubwa ya mazingira. Hayo ni kati ya mambo yanayowashangaza wangalizi wanaojiuliza iwapo hiyo ndiyo siasa inayofuatwa na serikali ya mseto ya SPD na chama cha Mazingira. Kisha si mwengine isipokuwa Waziri wa Mambo ya Uchumi wa Ujerumani wa serikali hiyo ya mseto, Wolfgang Clement anayewekea vizingiti sheria inayoandaliwa kuhusu matumizi ya nishati za manufaa za kimaumbile. Na juu ya kuwa Waziri huyo ndiye mwanasiasa wa mbele mwenye kusisitiza umuhimu wa kukomesha mitindo ya misaada ziada, kila mwaka hulipa EURO biliyoni tatu ziada kugharimia uzalishaji wa makaa ya mawe. Kote duniani watafiti wa hali ya hewa wanawafikiana kwamba hata kama tutafanikiwa kuupunguza kwa sehemu muwafaka ujoto mkali , katika miaka 50 ijayo lazima moshi wa magari na migodi ya makaa ipunguzwe kwa nusu. Ndiyo maana kila EURO inayolipwa kugharimia uzalishaji wa makaa inachangia kuzidisha uchafuzi wa mazingira. Lakini maonyo hayo ya watafiti hayapuzwi tu katika sekta ya hifadhi ya hali ya hewa. Kwa muda wa miaka mingi watafiti wa bahari barani Ulaya wanapigania upunguzaji wa viwango vya uvuvi wa samaki aina ya Kabelyau kwa hoja kwamba aina yao inayomalizika imehatarika na baada ya miaka michache tu hapatakuwa na Kabelyau hata mmoja. Juu ya hivyo Mawaziri wa Mambo ya Uvuvi wa UU wameendelea kuruhusu kuvuliwa kiwango kile kile cha Kabelyau hapo mwaka jana. Hata hivyo kutoka Brussels kuna pia ripoti za kutia moyo. Kwa mfano siku za usoni itawezekana kuipunguza misaada ziada ya kilimo na kuitumia kugharimia kilimo cha manufaa kinachochangia hifadhi ya mazingira na ufugaji wa manufaa wa wanyama. Kuna pia habari njema katika sekta ya hifadhi ya bahari. Karibuni zitapigwa marufuku meli za mafuta zilizojengwa kutoka ukuta mmoja tu, wakati katika Bahari ya Pasifik mataifa 11 yamelitangaza eneo moja kubwa kama eneo la kuhifadhi nyangumi, huku Norway imejipatia uwezo wa kuhifadhi mwambao zake za maji matamu zenye utajiri mkubwa wa matumbawe kwa kuzuiya uzalishaji wa mafuta katika maeneo hayo ya kuvutia. Hata hivyo mafanikio hayo madogo hayawezi kuficha ukweli kuwa mwaka jana haukuwa mwaka mzuri wa kimazingira. Tukiishi katika enezi zinazotawaliwa na ugaidi, vita na migogoro ya kiuchumi, sekta ya hifadhi ya maizingira zamani imekwisha pigwa kumbo. Kwa hali yoyote lazima ukumbukwe umuhimu wa kuchukuliwa hatua za dharura ikiwa tumekusudia kikweli kuwaandalia dunia bora vizazi vya siku za usoni.