1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Israel

IDF ilionywa kabla ya kutokea shambulizi la Oktoba 7

Sylvia Mwehozi
18 Juni 2024

Shirika la habari la umma la Israel la Kan limeripoti kwamba maafisa wa jeshi wa nchi hiyo walipewa tahadhari na idara za kijasusi za ndani ya jeshi kuhusu uwezekano wa maandalizi ya shambulizi la Hamas.

https://p.dw.com/p/4hCuU
Israel -vita-Gaza-wanajeshi
Magari ya kivita ya jeshi la IsraelPicha: Jim Hollander/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Kwa mujibu wa shirika la habari la Kan, kitengo cha kijasusi cha jeshi la Israelkiliandaa muhtasari mnamo mwezi Septemba, mwezi mmoja kabla ya shambulio la Hamas ambalo lilichochea vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza. Limesema katika ripoti yake kwamba muhtasari huo wa kitengo nambari 8200 cha ujasusi, ulijumuisha maelezo kuhusu wapiganaji wa Hamas waliokuwa wakifanya mafunzo ya utekaji, mipango ya uvamizi wa vituo vya kijeshi na jamii za Waisraeli haswa katika maeneo ya kusini.

SomaMkuu wa ujasusi Israel ajiuzulu kwa kushindwa kuzuia shambulizi la Hamas la Oktoba 7

Israel-Gaza-vita- IDF
Wanajeshi wa jeshi la Israel IDFPicha: Mohammed Nasser/IMAGO

Kitengo hicho nambari 8200 ni idara ya jeshi la ulinzi la Israel IDF ambayo inahusika kukusanya taarifa za kijasusi lakini inaonekana kuwa taarifa hizo zilipuuzwa na maafisa wa ngazi ya juu. Muhtasari huo unaeleza kwamba wanamgambo wa Kipalestina walilenga kuwateka mamia ya watu, kwa mujibu wa ripoti za shirika la Kan na kuongeza kuwa "Idadi ya mateka inatarajiwa kuwa kati ya watu 200-250."

Kwanini Israel-Hamasi hawatatii wito wa kusitisha vita?

Shirika la habari la Kan, linasema mipango ya kushambulia vituo vya kijeshi na makazi na kuchukua hadi mateka wapatao 250, wakiwemo wanawake na watoto, ilisambazwa ndani ya kitengo cha Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) kinachohusika na Gaza mnamo Septemba 19. Hali mbaya zaidi inayozingatiwa katika ripoti hizo ni kwamba magaidi kadhaa walikuwa na uwezo wa kuingia ndani ya Israel.

Mwandishi wa habari wa kijeshi wa shirika hilo la Kan anasema kuwa "mfumo wa ulinzi kwa wakati huo ulikuwa ukifanya kazi kuelekea kutuliza Ukanda wa Gaza, kwa njia ya kuboresha hali ya maisha ya raia, vibali vya kufanya kazi kwa Wapalestina na kuondolewa kwa vizuizi katika bidhaa."Hali ilivyo Gaza: Utulivu wa kiasi waripotiwa Gaza kufuatia usimamishaji mapigano wa muda

Kulingana na mwandishi huyo, IDF ilikuwa inategemea pakubwa ulinzi wa mipakani lakini kila kitu kilianguka mnamo Oktoba 7 na kwamba maafisa waandamizi katika kitengo kinachohusika na Gaza ndani ya jeshi hilo walipuuzia taarifa hizo za kijasusi. Ripoti za shirika la habari la Kan, zilizowanukuu maafisa wa usalama ambao halikuwataja majina, zinasema kuwa muhtasari juu ya uwezekano wa shambulizi la Hamas, zilisambazwa kwa kitengo cha Gaza na kile cha kamandi ya kusini ndani ya jeshi la IDF.

Wanasiasa wa Israel wamepuuzia miito ya uchunguzi wa kina kuhusu kushindwa kwa duru za kijasusi kuhusu shambulizi la Hamas la Oktoba 7, huku waziri mkuu Benjamin Netanyahu akisisitiza kwamba uchunguzi wowote utasubiri vita itakapomalizika ambavyo sasa viko mwezi wake wa tisa. Jeshi la Israel hata hivyo limelieleza shirika la habari la AFP kwamba "linachunguza matukio" ya Oktoba 7, na kwamba uchunguzi unaendelea na matokeo yake yatawekwa hadharani baadaye.

Israel -Tel Aviv
Baadhi ya mateka waliokombolewa na jeshi la IsraelPicha: Marko Djurica/REUTERS

Shambulio la kushutukiza la Hamas la Oktoba 7 lilisababisha vifo vya watu 1,194 wengi wakiwa ni raia kulingana na takwimu rasmi za Israeli. Wanamgambo hao wa Hamas pia waliwateka watu 251, ambapo hadi kufikia sasa 116 kati yao bado wanashikiliwa huko Gaza ikiwemo 41 waliokufa.

Israel ilijibu shambulizi hilo kwa operesheni kubwa ya kijeshi na tangu Oktoba 7 imewaua watu 37,349 katika Ukanda wa Gaza wengi wakiwa ni raia kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayoongozwa na Hamas.