1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Zelensky aomba silaha zaidi kwa washirika wake.

6 Septemba 2024

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ameshiriki mkutano nchini Ujerumani uliowakusanya waungaji mkono wa kimataifa wa nchi yake.

https://p.dw.com/p/4kMFC
Rais Volodymyr Selenskyj
Rais Volodymyr SelenskyjPicha: Heiko Becker/REUTERS

 Mkutano wa Ramstein unalenga  kuipa nguvu Kiev, siku kadhaa baada Urusi kufanya shambulio baya zaidi dhidi ya nchi hiyo.

Mkutano wa wadau wa kimataifa wanaoiunga mkono Ukraine unaongozwa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ramstein iliyoko Kusini Magharibi mwa mji wa Frankfurt hapa Ujerumani. 

Waziri huyo wa Ulinzi wa Marekani  ameshasema kwamba Washington itatowa msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine wa dola milioni 250.

Na mkutano huo umewaleta pamoja wajumbe kutoka kiasi mataifa 50 ukijikita kuyatazama masuala kadhaa ikiwemo kuimarisha mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine pamoja na kuwashawishi washirika wa nchi hiyo kuongeza nguvu sekta zao za silaha.

Waziri wa ulinzi  Lloyd Austin,na rais  Volodymyr Selenskyj na waziri wa ulinzi wa Ukraine Rustem Umerow
Mkutano wa RamsteinPicha: Heiko Becker/REUTERS

Zelensky aomba msaada zaidi

Rais Zelensky kwenye mkutano huo amewahimiza washirika wa nchi yake kuendelea kuipatia msaada zaidi wa silaha
 

"Ndio tunashukuru, tunashukuru sana kwa msaada mnaotupatia Ukraine, unaotolewa na nchi zenu. Lakini tunahitaji silaha zaidi ili kuviondowa vikosi vya Urusi kwenye ardhi yetu na hasa katika mkowa wa Donetsk.''

Zelensky pia amezitaka nchi washirika wake kupuuzia onyo la mstari mwekundu uliowekwa na Urusi na kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za masafa marefu kuishambulia ardhi ya Urusi.

Ni mkutano ambao pia unafanyika siku chache baada ya Urusi kufanya shambulio baya zaidi ndani ya Ukraine,lililouwa watu 55  na 300 wakajeruhiwa kwenye mji wa Poltava.

Taarifa zinasema  vikosi vya Urusi  vimeshausogelea mkoa wa Donbas kwa hivi sasa na Jana Alhamisi rais Vladmir Putin alitangaza kwamba lengo lake kubwa ni kulinyakuwa eneo hilo la mashariki mwa Ukraine katika vita hivi. 

Ukraine hii leo imedai imekombowa sehemu kadhaa za mji wa mashariki unaoitwa New-York katika kile kinachoonekana kuwa mafanikio yake ya mwanzo katika mapambano haya mapya.Soma pia:Zelensky anatazamiwa kukutana na Kansela Olaf Scholz

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani,Pentagon  Meja jenerali Pat Ryder amesisitiza kwamba Ukraine ni muhimu kwa nchi hiyo na usalama wa kimataifa na kwahivyo juhudi za washirika wa Kiev katika mkutano wa Ramstein zinaendelea kuwa na dhima muhimu kwenye vita vya Ukraine vya kupigania uhuru na mamlaka yake.

Baada ya mkutano huo Rais Zelensky pia atakutana  na Kansela Olaf Scholz kabla ya kuelekea baadae nchini Italia ambako atakuwa na mazungumzo na waziri mkuu Giorgia Meloni  na atashiriki pia mkutano wa kimataifa wa jukwaa la kiuchumi.

Ujerumani ni mchangiaji wa pili mkubwa kwa Ukraine lakini nayo hivi sasa iko kwenye shinikizo la ndani kuhusiana na suala la kuipatia msaada Kiev.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani  Boris Pistorius
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris PistoriusPicha: Andreas Arnold/dpa/picture alliance

Uchaguzi wa majimbo mawili  ya kile kilichokuwa kikijulikana kama Ujerumani Mashariki,Saxony na Thuringia uliofanyika hivi karibuni ulivipa nguvu vyama vya misimamo mikali ya kulia na kushoto ambavyo vinapinga kabisa hatua ya serikali ya kuisadia Ukraine. Soma pia: Bunge la Ukraine lakubali kujiuzulu kwa Kuleba

Marekani nayo muungaji mkono mkubwa wa Ukraine katika mapambano yake dhidi ya Urusi ambayo imeshaipatia nchi hiyo msaada wa dola bilioni 56 kwa sasa pia kuna mashaka yaliyoongezeka kuhusu hatma ya msaada huo baada ya uchaguzi wa rais wa Novemba ikiwa Donald Trump rais wa zamani wa nchi hiyo, atarudi madarakani.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW