Marais wawili wa Comoro wahusishwa katika kashfa ya pasipoti
18 Aprili 2018Ripoti hiyo ya bunge imetaka mahakama ichukuwe jukumu la kushughulikia matukio hayo ya ubadhirifu wa fedha za umma na kula njama ambapo marais hao wawili wa zamani wamehusishwa.
Kashfa hiyo inaanzia nyuma mwaka 2008 wakati Comoro ilipoanzisha mpango kwa kushirikiana na Umoja wa falme za Kiarabu na Kuwait, kuwapa uraia wakaazi wa falme hizo mbili za Ghuba wa jamii ya Mabedui ambao hawatambuliwi kuwa na utaifa wa nchi yoyote. Badala yake Comoro ilitarajiwa kupokea vitega uchumi muhimu kutoka mataifa hayo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.
Makubaliano ya awali ni kwamba familia 4,000 za mabedui zingepewa urai wa Comoro na visiwa hivyo kulipwa dola 163 milioni, ambazo zingetumiwa katika miradi ya miundo mbinu.
Mnamo miaka iliofuata karibu hati 48,000 za kusafiria zilitolewa, lakini kwa mujibu wa utafiti wa bunge ni pasipoti chache tu walizopewa mabedui. Pasipoti 6,000 lakini ziliuzwa nje ya utaratibu wa kisheria. Ripoti imesema hati hizo ziliuzwa kimagendo. Mpwa wa rais wa zamani Sambi aliweza kwenda kuchapisha pasipoti nyingi atakavyo, kwa mkataba na kampuni moja ya Ubeligiji.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa bunge, sehemu kubwa ya malipo ya paspoti kati ya 25,00 na 200,000 ziliibiwa. Kwa jumla sehemu kubwa ya fedha hazikuonekana kwenye hazina ya serikali. Serikali inafikiwa kupoteza hadi dola 971 milioni, karibu 80 asilimia ya pato jumla la taifa. Rais wa zamani Sambi alipokea kiinua mgongo cha hadi dola milioni 105 kwa kusaini mkataba huo.
"Tunachotarajia, nafikiri wacomoro wote, wanademokrasia wote wanahitaji maelezo ya kina. Ninaamini viongozi wa nchi watawajibika," amesema Naibu Spika wa bunge la taifa Dhahir Zulkamal, akizungumza na DW juu ya kile wanachotarajia.
Sambi na Ikililou aliyemrithi Urais, wote wamekanusha kuhusika na kashfa hiyo mmoja wa mawaziri wake wa zamani Ahmed Barwane alisema Sambi hakuwahi kuona chochote kuhusiana na kashfa hii.
Mradi huo wa pasipoti kwa ajili ya vitega uchumi , sasa umesimamishwa na Rais Azali Assoumani mara tu aliposhinda uchaguzi uliopita 2016. Azali alikabidhiwa ripoti ya bunge wiki iliopita na Spika Abdou Ousseni ambaye aliliambia gazeti la serikali Al-watan, kwamba jukumu lao lilikuwa ni kujuwa kilichotokea, kitakachofuata sasa ni uamuzi wa uongozi wa juu wa taifa na mahakama.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp
Mhariri: Mohammed Khelef