1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Senegal Sall hatowania muhula wa tatu

4 Julai 2023

Rais wa Senegal Macky Sall amehitimisha miezi kadhaa ya sintofahamu kwa kusema kuwa hatogombea kwa muhula wa tatu mwaka ujao. Hatua hiyo inasafisha ya kufanyika uchaguzi wa wazi katika taifa hilo la Afrika Magharibi

https://p.dw.com/p/4TNLe
Frankreich | Senegals Präsident Macky Sall
Tangazo la Sall linafuatia miezi kadhaa ya tetesi kuwa anapanga kugombea kwa muhula wa tatuPicha: Lewis Joly/AP/picture alliance

Sall kufikia jana alikuwa amesalia kimya kuhusu azma yake, na kuzusha hofu kuwa angetumia mabadiliko ya katiba kuurefusha ukomo wa mihula miwili. Sall alisema uamuzi wake baada ya tafakari ya muda mrefu ni kutokuwa mgombea katika uchaguzi wa Februari 25 mwaka wa 2024.

Soma pia: Sonko awataka Wasenegal kujitokeza kwa wingi kabla ya hotuba ya rais

Katika hotuba ya jana usiku kwa njia ya televisheni, Rais huyo alisema alitaka kuweka kipaumbele maendeleo ya nchi yake, na hasa katika wakati ambao kuna matatizo ya kijamii na kiuchumi. Alisema hata kama ana haki ya kugombea, alihisi kuwa jukumu lake sio kuchangia katika kuharibu kile alichokijenga kwa nchi hiyo. Kwamba alisema muhula wake wa 2019 ungekuwa wake wa mwisho. Anafahamu uamuzi huo umewashangaza wote walio na urafiki naye. Anasema Senegal ni muhimu kumliko, na imejaa viongozi wenye uwezo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Katika mkesha wa hotuba hiyo ya taifa, mkosoaji wake mkubwa, Ousmane Sonko, alikuwa ameuhimiza umma kujitokeza kwa wingi na kumpinga. Makabiliano makali yalizuka mwezi uliopita kati ya wafuasi wa Sonko na vikosi vya usalama, na kusababisha vifo vya watu 16.

Ousmane Sonko
Sonko alipewa kifungo cha miaka miwili jelaPicha: Fatma Esma Arslan/AA/picture alliance

Machafuko hayo yalitia doa taswira ya Senegal kuwa ngome ya utulivu katika eneo la Afrika Magharibi, ambalo limefahamika kwa mapinduzi ya mara kwa mara na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Sall alichaguliwa rais wa Senegal kwa mara ya kwanza mwaka wa 2012 baada ya kumpiku aliyekuwa rais wa wakati huo Abdoulaye Wade, ambaye uamuzi wake wa kugombea kwa muhula wa tatu wenye utata ulizusha maandamano yenye vurugu. Wade hatimaye alikiri kushindwa baada ya duru ya pili ya uchaguzi kati yake na Sall. 

Marekebisho ya katiba

Katika mwaka wa 2016, Sall aliirekebisha Katiba na kuweka ukomo wa mihula miwili ya urais. Wafuasi wake walisisitiza kuwa muhula wake wa kwanza chini ya katiba ya awali usingehesabika.

Katika hotuba yake ya Jumatatu usiku, Sall aliiomba serikali kufanya kila liwezekanalo kuandaa uchaguzi wa wazi Februari mwakani. Haikufahamika mara moja nani atakayegombea kwa tiketi ya chama cha kisiasa cha Sall.

Viongozi wa kikanda, wakiwemo marais wa Niger, Mohamed Bazoum, Umaro Sissoco Embalo wa Guinea Bissau, na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat waliusifu uamuzi wa Sall, wakati Bazoum akiongeza kuwa utapunguza hofu.

Wafuasi katika makao makuu ya chama mjini Dakar walionekana kugawanyika baada ya hotuba ya Sall. Baadhi waliipongeza wakati wengine wakilia.

Marais kadhaa wa Kiafrika tayari wamajaribu kubaki madarakani katika miezi ya karibuni kwa kuzibadilisha katiba zao kwanza, wakiwemo Alassane Ouattara wa Cote d'Ivoire, aliyeshinda muhula wa tatu mwaka wa 2020. Mwingine, Alpha Conde wa Guinea, alishinda muhula wa tatu mwaka huo pia lakini hakukaa sana: Mapinduzi ya kijeshi yalimuondoa madarakani chini ya mwaka mmoja baadae.

Afp, ap, reuters