1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sonko awataka Wasenegal kujitokeza kabla ya hotuba ya rais

3 Julai 2023

Kiongozi maarufu wa upinzani nchini Senegal Ousmane Sonko ametoa wito kwa umma kujitokeza kwa wingi kabla ya hotuba ambayo Rais Macky Sall anatarajiwa kutangaza kama atawania muhula wa tatu wenye utata au la

https://p.dw.com/p/4TKwg
Senegal | Ousmane Sonko
Ousmane Sonko amezuiwa nyumbani kwakePicha: Seyllou/AFP/Getty Images

Katika hotuba yake ya kwanza tangu alipohukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, Sonko ameandika jana usiku kwenye mitandao ya kijamii kuwa lazima Wasenegal wajitokeze kupambana na utawala wa Macky Sall na kumwambia kuwa hana dhamana ya kuwachagua wagombea watakaoshindana katika uchaguzi ujao wa rais.

Soma pia: Senegal kuanzisha uchunguzi baada ya machafuko

Sonko alihukumiwa mapema mwezi Juni kifungo cha miaka miwili jela mwezi uliopita kwa kumpotosha msichana mdogo, uamuzi uliozusha maandamano yaliyosababisha vifo vya watu 16. Hukumu hiyo inamzuia kugombea katika uchaguzi wa rais wa mwaka ujao. Alidai kuwa kesi hiyo ya mahakamani ilitengenzwa kumzuia kugombea urais, madai ambayo maafisa wanakanusha. Sonko amemlaumu Rais Sall kwa matatizo yanayoikumba nchi "Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, matukio ya kusikitisha na yenye uchungu yamefuatana kwa kasi ya kutisha, pamoja na mauaji, vifungo vya kiholela na uharibifu wa mali. Yote haya, wananchi wenzangu, ni kwa sababu ya tamaa ya mtu mmoja tu ya madaraka."

Senegalese President Macky Sall
Sall alichaguliwa mara ya kwanza 2012 na tena 2019Picha: Presidency of Senegal / Handout/AA/picture alliance

Amefungiwa na mamlaka nyumbani kwake tangu Mei 28. Wakati huo huo, Sall anatarajiwa kutangaza leo usiku kama atawania au la baada ya kuiweka nchi hiyo katika sintofahamu kuhusu azma yake kwa miezi kadhaa. Alichaguliwa mara ya kwanza 2012 na tena 2019.

Katiba inasema rais hawezi kuhudumu kwa zaidi ya mihula miwili, lakini wafuasi wake wanataka agombee tena wakihoji kuwa marekebisho ya katiba katika mwaka wa 2016 yalianzisha upya sheria hiyo.

Soma pia: Senegal: Utulivu warejea baada ya maandamano yenye ghasia

Sonko amesema jana kuwa iwapo atakamatwa na asiwachiliwe ndani ya saa mbili, anatoa wito kwa watu wa Senegal kusimama kama kitu kimoja na kujitokeza kwa wingi na mara hii kuuwekea kikomo utawala wa uhalifu. Amesema kama rais atatangaza nia yake ya kugombea kwa muhula wa tatu, itakuwa juu ya watu wote wa Senegal kusimama na kumkabili.

Aliuhimiza umma kukusanyika na kudai kuwachiliwa huru kwa wafungwa wa kisiasa na kukomesha haraka iwezekanavyo kile alichokiita "kuzuiliwa kwake na serikali bila mashitaka”

Mwanasiasa huyo wa upinzani pia amedai kuwa mazungumzo ya karibuni ya kitaifa yaliyoanzishwa na Sall ambayo yalirejesha mwelekeo wa kisiasa wa viongozi wengine wawili waliokuwa wametengwa hapo awali ilikuwa ni mpango uliolenga kumnyima hata Zaidi fursa ya kuingia Ikulu.

Mwishoni mwa wiki, alihudhuria mkutano wa maafisa wa serikali ya mitaa waliomkabidhi waraka wa kumuunga mkono. Alisema mapambano yake na Fahari yake kubwa ni kupata ushindi na kutekeleza sera za kiuchumi kwa manufaa ya wananchi.

afp