1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais EU akutana na waziri mkuu India Narendra Modi

Alex Mchomvu25 Aprili 2022

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, wametangaza kuzinduliwa kwa Baraza maalum la kuimarisha Biashara na Teknolojia baina ya EU na India.

https://p.dw.com/p/4AQ1K
Indien - Ursula von der Leyen in Dehli mit Narendra Mod
Picha: REUTERS

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen leo Jumatatu amekutana na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi katika mji mkuu, New Delhi,licha ya viongozi hao wawili kuwa na mitazamo tofauti juu ya uvamizi wa Urusinchini Ukraine.

Viongozi hao wawili walitangaza makubaliano hayo ya kuzinduliwa kwa Baraza la Biashara na Teknolojia ili kushirikiana katika masuala ya teknolojia na usalama.

Soma zaidi:Wang Yi afanya ziara rasmi India

Wamesema makubaliano hayo ni hatua muhimu kuelekea ubia wa kimkakati ulioimarishwa kwa washirika wote wawili ili kukabiliana na changamoto katika sekta ya biashara, teknolojia inayoaminika na usalama.

Baraza latarajiwa kutoa mwelekeo wa kisiasa na kimuundo

Baraza hilo la Biashara na Teknolojia litatoa mwelekeo wa kisiasa na muundo muhimu wa kufanya maamuzi ya kisiasa na pia kuratibu kazi ya kiufundi na kutoa ripoti kwa ngazi ya kisiasa ili kuhakikisha utekelezaji na ufuatiliaji katika maeneo ambayo ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya uchumi.

Indien l Präsidentin der Europäischen Kommission Ursula von der Leyen in Gurgaon
Ursula von der Leyen akiwa na akiwa na Vibha Dhawan,katika mjadala wa masuala ya mazingira IndiaPicha: Money Sharma/AFP

Wakati wa kuhitimisha taarifa hiyo ya pamoja, walieleza kuwa wanapoadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia, kuna uhakika kwamba maadili ya pamoja na maslahi ya pamoja ya Umoja wa Ulaya na India yanatoa msingi thabiti wa kuimarisha manufaa kwa pande zote.

Soma zaidi:Umoja wa Ulaya waanza kujiwekea dawa za kukabiliana na athari za mionzi

Hatua ya kuunda Baraza la Biashara na Teknolojia ni ya kwanza kwa India na ya pili kwa Umoja wa Ulaya. Umoja wa Ulaya tayari umeweka makubaliano sawa na haya na Marekani.

 

Umoja wa Ulaya inaimarisha zaidi mahusiano na India

Umoja wa EU, kama ilivyo Marekani na Uingereza, kwa sasa inafanya juhudi ya kuboresha uhusiano na India, nchi ya pili duniani yenye idadi kubwa ya watu.

Frankreich | EU Gipfel in Versailles | Ursula von der Leyen
Ursula von der Leyen katika majukumu ya kikazi ya Umoja wa UlayaPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Licha ya ongezeko la shinikizo kutoka viongozi mbalimbali duniani wanaoitaka India kukata uhusiano wake na Urusi, nchi hiyo bado inaendelea kudumisha uhusiano wa karibu wa kidiplomasia, kibiashara na kijeshi na Urusi, huku ikiendelea kununua mafuta ya bei nafuu kutoka kwa mshirika wake huyo huku  nchi za Magharibi zikiiekea Moscow vikwazo baada ya uvamizi wake nchini Ukraine.

Soma zaidi:Ulaya na China kushirikiana kuleta amani ulimwenguni

Hata hivyo von der Leyen na Modi hawakutoa taarifa ya pamoja juu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine

Katika mahojiano mwishoni mwa juma, Waziri wa Fedha wa India Nirmala Sitharaman aliiambia shirika la habari la Bloomberg News kwamba India inataka kuwa marafiki na Umoja wa Ulaya na nchi za Magharibi lakini si kama rafiki dhaifu anayehitaji misaada ya hapa na pale.