1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi kutathmini azimio kutaka MONUSCO kuondoka DRC

2 Agosti 2022

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Felix Tshisekedi ameongoza kikao ambacho kitatathimini azimio la kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, kuondoka hatua kwa hatua.

https://p.dw.com/p/4F0PN
Felix Tshisekedi | Präsident Demokratische Republik Konogo
Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Hatua hiyo ameifikia baada ya kupokea ripoti kutoka kwa wajumbe wake aliowatuma Goma na Butembo kuwatuliza waandamanaji, ambao waliandamana kwa muda wa wiki moja ya kukipinga kikosi hicho mashariki ya Kongo. 

Kwenye tangazo lililotolewa na Patrick Muyaya, msemaji wa serikali ya Kongo, Rais Tshisekedi ameiomba serikali kuandaa mkutano na wajumbe wa tume ya MONUSCO ili kwa pamoja watathmini mpango wa kuondoka kwa kikosi hicho nchini Kongo, kulingana na azimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 2556.

Tshisekedi azungumza na Guterres

Katika kikao kilichofanyika Jumatatu mjini Kinshasa, Rais Tshisekedi alisema, kuwa alizungumza kwa njia ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliyempatia salamu za rambirambi ya vifo vilivyotokana na maandamano yaliyofanyika nchini Kongo.

Akimpa pia pole kufuatia vifo vya askari wanne wa MONUSCO, rais wa Congo alimuomba Guterres kuhakikisha kwamba uchunguzi unafanyika ili kuwaadhibu askari wa Umoja wa Mataifa waliohusika kwenye mkasa wa Jumapili mjini Kasindi. 

Demokratische Republik Kongo | Goma | Proteste gegen UN
Maandamano katika mji wa Goma ya kuitaka MONUSCO kuondoka KongoPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Hatua ya kutathmini mpango wa MONUSCO kuondoka Kongo imepokelewa vyema na baadhi ya wakaazi wa eneo hilo, ambao wanadhani kwamba, licha ya watu waliouawa wakati wa maandamano, waandamanaji wamefikia malengo yao ambayo ni kuona kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Kongo kinaondoka nchini humo.

Na huko hayo yakijiri, mashirika ya kiraia ya mkoa wa Kivu ya Kaskazini, yametangaza matokeo ya maandamano ya siku saba mfululizo dhidi ya MONUSCO, na kuliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiondoa tume yake Kongo mapema iwezekanavyo.

Mashirika ya kiraia: Wananchi hawaitaki MONUSCO

Edgar Mateso, naibu mratibu wa mashirika hayo, amesema raia hawawataki tena askari wa MONUSCO na hivyo linalitaka baraza hilokuwaondoa mapema. ''Tunalitaka baraza hilo lianzishe uchunguzi Goma, Kanyabayonga, Butembo, Beni na Kasindi kuwakamata askari wa Umoja wa Mataifa na viongozi wao waliowafyatulia risasi waandamanaji na hiyo ili sheria ifuate mkondo wake pamoja na kuzilipa fidia familia za wahanga," alisisitiza Mateso.

Wakaazi Kivu washinikiza kuondolewa MONUSCO DRC

Kwa upande wake, mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mji wa Butembo, Pasta Mathe Saanane, amewaomba wakaazi wa Butembo kuendelea na shughuli zao za kawaida, akitangaza kuvunjwa kwa uhusiano baina ya mashirika ya kiraia na MONUSCO. Na wakati taarifa hii ikiandaliwa, hali ni tulivu katika maeneo mbalimbali yaliyoshuhudia maandamano kwa lengo la kukitaka kikosi cha MONUSCO kuondoka nchini Kongo.