1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya Somalia ataka maridhiano ili kujenga amani

30 Mei 2022

Rais mpya wa Somalia amesifu kurejea kwa wanajeshi wa Marekani kusaidia kupambana dhidi ya waasi na anasema kurejesha usalama kunategemea maridhiano na viongozi wengine wa Somalia.

https://p.dw.com/p/4C3j2
Somalia Präsident Hassan Sheikh Mohamud
Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden mwezi huu aliidhinisha kutumwa tena kwa mamia ya wanajeshi wa Marekani ambao watasaidia kutoa mafunzo, kuandaa na kuunga mkono kikosi maalumu cha kijeshi cha Danab kinachopambana na wanamgambo wa al Shabaab wenye mafungamano na al Qaeda.

Rais Donald Trump aliwaondoa wanajeshi hao mnamo Desemba 2020, na kuwaacha wakiingia na kutoka kwa kazi maalumu kutokea nchi jirani ya Kenya, hatua ambayo wataalam walielezea kuwa ya gharama kubwa na hatari.

"Tunashukuru sana kwa Rais Biden kurudisha baadhi ya vikosi ... daima vimekuwa vikishiriki katika vita dhidi ya al Shabaab," Rais Hassan Sheikh Mohamud aliiambia Reuters, akiongeza kwamba alitaka uungwaji mkono wa Marekani uendelee.

Soma pia: Hassan Sheikh Mohamud arejea kuwa rais wa Somalia

Kundi la Al Shabaab limewaua makumi ya maelfu ya Wasomali katika mashambulizi ya mabomu mjini Mogadishu na kwingineko wakati likijaribu kuiangusha serikali, pamoja na raia katika nchi jirani katika mashambulizi dhidi ya maduka makubwa, hoteli, chuo kikuu na migahawa.

Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Rais mpya Somalia Hassan Sheikh Mohamud.Picha: Abukar Mohamed Muhudin/AA/picture alliance

Wabunge wa Somalia walimchagua Mohamud kama rais mwezi Mei - nchi hiyo haijafanya uchaguzi wa mtu mmoja - kura moja tangu kuzuka kwa

vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka wa 1991.

Wabunge walizuia majaribio ya rais aliyepita kuongeza muda wake, lakini suala hilo lilivigawanya sana vikosi vya usalama, ambavyo vilipambana katika mitaa ya mji mkuu.

Mgogoro huo wa muda mrefu uliondoa tahadhari kutokana na kuongezeka kwa dharura ya kibinadamu na kulazimisha zaidi ya Wasomali milioni 6 kutegemea msaada wa chakula.

Soma pia: Wabunge wa Somalia kumchagua rais mpya

James Swan, afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, alisifu uteuzi wa Mohamud wa mwanasiasa mashuhuri kushughulikia hali ya dharura, iliyochochewa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 40.

Kipaumbele cha juu

Tangu ushindi wa Mohamud mnamo Mei 15, akaunti rasmi za mitandao ya kijamii za serikali zimetoa picha zake akiwakaribisha wapinzani wa zamani wa kisiasa na viongozi wa mikoa ya Somalia, ambao wengi wao walishiriki makabiliano ya silaha na mtangulizi wake.

"Watu wanapaswa kusuluhisha," mwalimu huyo wa zamani Mohamud alisema akiwa ikulu ya Villa Somalia, ambayo ni jengo la serikali lililopakwa rangi za kitaifa, nyeupe na buluu.

Maneno ya Mohamud yamewatia moyo washirika waliokatishwa tamaa na maendeleo ya polepole chini ya mtangulizi wake, ambayo yaliruhusu uasi kupata nguvu.

Soma pia: Somalia baada ya kuchaguliwa Hassan Sheikh Mohamud kuwa rais

Luteni Jenerali Diomede Ndegeya, kamanda wa vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia, alisema anatumai vikosi vya ndani na tawala vinaweza kusaidia kuimarisha usalama wa barabara kwa vikosi vya AU na Somalia kupiga hatua dhidi ya al Shabaab.

"Ni muhimu kwetu sote kufanya kazi pamoja," alisema.

Shambulio kubwa la mwisho dhidi ya al Shabaab lilikuwa mwaka 2019. Waasi hao bado wanadhibiti maeneo mengi nchini humo lakini vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika vinatarajiwa kuondoka katika kipindi cha miaka mitatu.

Mwezi huu, al Shabaab walivamia kambi ya walinda amani wa AU, na kuua makumi ya wanajeshi. Burundi imetaja idadi ya waliofariki kuwa 10.

"Kipaumbele chetu kikuu ni usalama," alisema Mohamud, ingawa aliorodhesha mambo mengine ya dharura, ikiwa ni pamoja na kujenga taasisi na kuratibu sheria za uchaguzi na mamlaka ya serikali.

Soma pia: Somalia na matumaini ya enzi mpya kwa Hassan Sheikh Mohamud

Wakati Mohamud aliwahi kuwa rais, kuanzia 2012-2017, rushwa iliyokithiri ililijaza jeshi na askari hewa. Wale waliokuwepo mara nyingi waliuza bunduki zao wakati mishahara yao ilipoibiwa.

Kutana na Fathi Muktar, kapteni wa walinzi wa ufuoni Somaliland

Tangu wakati huo, Umoja wa Mataifa umeanzisha kanzudata iliyopangwa kwa muda mrefu ya biometriska. Wanajeshi na watumishi wa umma sasa wanapokea mishahara yao moja kwa moja kwenye akaunti zao za benki.

Mohamud alikiri juu ya malalamiko ya mara kwa mara ya rushwa, lakini akapongeza uboreshaji wa kidijitali na kusema alipanga kuendeleza mageuzi ya kifedha ambayo hapo awali alisaidia kuyajadili na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa.

"Sote tunaunga mkono mageuzi ya kiuchumi," alisema.

Wanaharakati wanasema uthitbisho utakuwa endapo wanaomuunga mkono watapata kandarasi nono au nafasi za juu wanazotumia kupata malipo ya hongo.

"Tunahitaji ukaguzi wa kodi zote zilizokusanywa mjini Mogadishu, tunahitaji kulipa mishahara kwa wakati na tunahitaji kuepukana na upendeleo," alisema Mohamed Mubarak, mwanzilishi wa kundi la kupambana na rushwa la Marqaati.

Chanzo: RTRE