1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia yajiandaa kwa uchaguzi licha ya hofu ya usalama

12 Mei 2022

Somalia inatarajia kufanya uchaguzi wa rais Jumapili ijayo na kuhitimisha mchakato mgumu wa uchaguzi ambao umezidisha mivutano nchini humo baada ya muhula wa rais kumalizika bila kuwepo mtu wa kuchukua nafasi yake.

https://p.dw.com/p/4BC2H
Somalia Mogadischu Parlament
Wabunge nchini Somalia katika majengo ya bunge mji mkuu wa MogadishuPicha: Sadak Mohamed/AA/picture alliance

Mamlaka husika imeorodhesha watu 39 waliotangaza nia ya kugombea wadhifa huo, akiwemo rais wa sasa Mohamed Abdullahi Mohamed.

Kwenye orodha hiyo  wapo pia marais wengine wawili wa zamani, mwanasiasa aliyekuwa waziri mkuu na maafisa kadhaa wengine wa ngazi za juu na hata waandishi wa habari.  

Kadhalika mchuano huo utamjumuisha mwanamke mmoja Fawzia Yusuf Haji Adam ambaye ni mbunge na aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Somalia.

wabunge na maseneta ambao ndiyo watamchagua kiongozi mkuu wa nchi watapiga kura katika eneo lenye ulinzi mkali lililo katika uwanja wa ndege mjini Mogadishu.