Rais Kenyatta ahutubia bunge Kenya
30 Novemba 2021Hotuba hiyo ya pili kufanyika chini ya wingu la COVID 19 imetolewa mbele ya kikao cha pamoja cha wabunge 94 na maseneta 26 pekee kwa kuzingatia vikwazo vya kuzuwia virusi kusambaa.
Viongozi wa kisiasa waliweka kando tofauti zao na kukaa pamoja bungeni.
Hii ni hotuba yake ya mwisho mwaka huu kabla ya wabunge kuelekea kwenye mapumziko kuanzia tarehe 2 Disemba.
Viongozi wa ngazi ya juu serikalini akiwemo Naibu wa Rais William Ruto, kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM Raila Odinga aliyesindikizwa na wenzake wa upinzani Musalia Mudavadi na Kalonzo Musyoka kadhalika Jaji Mkuu Martha Koome walihudhuria kikao hicho cha kilele.
Soma: Kenyatta afuta mkutano mkuu wa chama cha Jubilee
Akilihutubia taifa kwa mara ya 8, Rais Uhuru Kenyatta alifafanua kuwa kifurushi cha kwanza cha kusisimua uchumi kilichowasili wakati baa la covid 19 lilipotua kiliyapunguza makali yake. Alishikilia kuwa hatua ilizochukua nchi zililenga kuyanusuru maisha na kuufufua uchumi.
Kiongozi wa Kenya alikumbushia ilikoanza safari yake ya siasa na waliomtangulia bungeni na kusisitiza kuwa kiongozi analazimika kuwajibika pasina kujali msimamo wa kisiasa.
Soma: Ruto tayari kuzungumza na Kenyatta bila masharti
Kwenye suala la elimu, madarasa alfu 10 mapya yaliweza kujengwa katika kipindi hicho japo hayajakamilika.
Rais Uhuru Alibainisha pia kuwa uchumi wa Kenya ulikua kwa 0.3% katika kipindi cha mwaka 2020 wakati ambapo madhila ya COVID 19 yalikuwa yanauvuruga ulimwengu.
Kenyatta alisisitiza kuwa linapozuka janga, mawili hutokea, ima ni kujawa na hofu na kuangamia au kuona nafasi za kujijenga upya na kuhimili dhoruba. Wakenya wana hisia mseto kuhusu hali ya uchumi.
Kwenye sekta ya afya, amesema vitengo vya kuwahudumia wagonjwa mahututi viliongezeka ili kuwatibu walioambukizwa COVID 19 na magonjwa mengine.
Soma: Uhuru atangaza sheria mpya kudhibiti corona kanda ya Ziwa na Bonde la Ufa
Kadhalika serikali iliweza kutenga zaidi hela kuwaajiri wahudumu wa ziada wa afya na kulipia huduma za jumla.
Wakati ambapo aina tofauti ya virusi vya COVID 19 vimegunduliwa, Kiongozi wa taifa aliyarai mataifa ya kigeni kutofunga mipaka yao kwani sio suluhu ya kuzuwia usambaaji. Hata hivyo aliusisitizia umuhimu wa wakenya kuchanjwa.
Kufikia sasa watu milioni 7.1 wamepokea chanjo ya COVID 19.Hotuba hii ya taifa imefanyika wakati ambapo uchaguzi mkuu unasubiriwa kufanyika mwakani.
Mwandishi: TM,DW Nairobi.
Mhariri: Daniel Gakuba