1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta afuta mkutano mkuu wa chama cha Jubilee

Shisia Wasilwa
23 Novemba 2021

Rais Uhuru Kenyatta amefutilia mbali mkutano mkuu wa chama cha Jubilee ambao ulikuwa umepangiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.

https://p.dw.com/p/43NIo
Kenia Wahlkampf | Präsident Uhuru Kenyatta
Picha: Reuters/B. Ratner

Hatua hiyo ni afueni ya muda kwa makamu wa rais William Ruto ambaye alikuwa anatazamiwa kuondolewa chamani humo kutokana na uhasama kati yake na rais. Chama hicho ambacho kimesamabaratika, kimeendelea kuwapoteza wafuasi wake kwa makamu wa rais ambaye ameunda chama chake kipya cha United Democratic Alliance.

Hatua hiyo ya Rais Uhuru pia inaibua hali ya wasiwasi kuhusu mipango ya kuidhinisha rasmi ndoa kati ya chama cha Jubilee na chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga. Rais Uhuru ameonesha bila kuficha kuwa anamuunga mkono Raila ambaye wamekuwa wakishirikiana katika masuala ya siasa tangu wazike tofauti zao za kisiasa zilizozaa salamu za heri. Sekretariati ya muungano huo ilikuwa ifutwe kwenye mkutano huo mkuu ambao ulikuwa ukingojewa kwa hamu na ghamu. Makamu wa Rais William Ruto ameeleza kuwa chama hicho kilishazikwa.

"Sasa wanatusumbua na Jubilee nini? Wao ndio walimaliza chama, hawa watu wote walishahamia ODM, sisi wengine tumeenda UDA, sasa Jubilee ifungwe!”

Huku baadhi ya washirika wa rais wakisisitiza kuwa hatua ya kufutilia mbali mkutano huo mkuu wa chama inatokana na hotuba kwa taifa ambayo itatolewa mwisho wa mwezi huu, baadhi ya wabunge wa mrengo wa Kieleweke, wamesema kuna tatizo na kwamba mkutano hauwezi kuwa umeshapangwa kwa mwezi mzima kisha likafutiliwa mbali mara moja.

Kenia Wahlen Uhuru Kenyatta und William Ruto
Rais Kenyatta na makamu wake William RutoPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Waraka uliotolewa hivi karibuni ulifichua kuwa, chama hicho kilikuwa kinalenga kumteua mgombea mmoja kwenye uchaguzi mkuu ujao na kuwatimua wabunge 100 wanaogemea upande wa Ruto. Chama hicho kiliwatimua zaidi ya wakurugenzi 70 katika matawi ya sekreteriati yake kote nchini Kenya kama anavyofafanua Raphael Tuju ambaye ni katibu Mkuu wa chama cha Jubilee.

"Iwapo tumekubaliana, kwa misingi ya kuunda muungano, basi lazima tumchague mgombea mmoja wa urais wa Jubilee na ODM.”

Kuna hofu kuwa washirika wa rais wameamua kuwa uwamuzi wa kumtimua Ruto chamani, miezi tisa kabla ya uchaguzi mkuu huenda ukavuruga mipango ya rais ya kuachia madaraka. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa hatua ya kumtimua Ruto chamani ni dhihirisho la misingi mibovu ya vyama nchini kenya.

Wakati huo huo, Muungano wa Kenya Moja OKA umekanusaha madai kuwa miungano mingine ya siasa inautaka waungane kabla ya uchaguzi mkuu. Muungano huo umetaja kuwa ni ndoto kushirikiana na Raila ama Ruto. Naye kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karu,a na spika wa bunge la taifa, Justin Muturi, wameashiria kuwa watashirikiana na muungano wa Kenya Moja kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

"Oka na uongozi wa mlima Kenya, tumekuja pamoja kujadili njia za kushirikiana, sote ni Wakenya na hakuna anayeweza kufaulu pekee yake.”

Karua aliyasema hayo kwenye mkutano na viongozi wa OKA akiwemo Musalia Mudavadi wa ANC, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Moses Wetangula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu.