1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila afanya ziara nchini Uingereza

Shisia Wasilwa
14 Machi 2022

Mgombea urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga ameanza ziara ya siku tano nchini Uingereza, ambapo anatarajiwa kukutana na Waziri wa Masuala ya Ulinzi James Heappey na Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby.

https://p.dw.com/p/48RYq
Elfenbeinküste / Ouattara / Odinga
Picha: AP

 

Ziara yake Raila inajiri juma moja tu baada ya Naibu Rais Ruto, kukamilisha ziara yake ya siku 10 katika mataifa ya Marekani na Uingereza.

Ruto alitumia fursa hiyo kuupaka matope utawala wa Rais Kenyatta na kuelezea wasiwasi wake kuhusu mipango ya kuiba kura kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti, 9 mwaka huu.

Raila anatarajiwa kuitumia ziara hiyo kutengua matamshi ya Ruto yanayoonekana kuutia doa uchaguzi mkuu ujao.

Aidha, Raila anaondoka nchini akifahamu fika nafasi yake baada ya Kongamano la pamoja la wajumbe wa Muungano wa Azimio kumpa jukumu la kupeperusha bendera yake.

Soma pia: Kenya yaondoa masharti ya mwisho ya Covid-19

Vyama 22 vinavyounda Muungano huo, vilimpa Raila ridhaa hiyo vikiongozwa na Rais Kenyatta wa chama cha Jubilee.

"Sote tushirikiane tuwe kitu kimoja, hakuna mtu ataachwa nje ya serikali ya Raila Amollo Odinga. Wote watakuwa ndani."

Kesho Jumanne, Raila atakutana na Waziri wa Masuala ya Ulinzi James Heappey. Baadaye atakutana na balozi wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya biashara nchini Kenya Theo Clerk na kisha kutoa mhadhara katika taasisi ya maarufu ya Chatham House. Raila amesema atafuata nyayo za mtangulizi wake Rais Kenyatta.

"Wameamua kunipatia mimi kijiti, kukimbia nacho kwenye kinyang'anyiro, ambacho kitakuja tarehe tisa mwezi wa nane, mwaka huu. Nimewahakikishia kuwa hiki kijiti nitakimbia nacho kwa ushujaa na kuleta ushindi."

Wakati huo huo, naibu rais William Ruto alikuwa mtu mwenye huzuni na ghadhabu alipoandaa mkutano mkubwa wa Kenya Kwanza katika ngome ya Rais Kenyatta, ya Kiambu. Ruto pamoja na washirika wake, walishikilia kuwa ajenda nne kuu za serikali ya Jubilee zilisambaratika kwa sababu rais alitia nguvu nyingi kwenye siasa za urithi.

Soma pia: Tume ya uchaguzi Kenya yashindwa kufikia malengo ya usajili

Alilitaja chaguo la rais kwa kiongozi wa ODM, kuwa bovu na litakaloshindwa, kwani atajali na kuyalinda maslahi ya wachache. 

"Sisi ambao unatudhulumu, sisi unaotupiga vita, mimi nataka nikuambie mheshimiwa ndugu yangu Rais, tumeona unavyotufanya, lakini kwa sababu sisi ni wacha Mungu, tumekusamehe."

Ruto aliitumia fursa hiyo kuupigia debe mfumo wake wa kuwajumuisha walala hoi serikalini, iwapo atafanikiwa kuwa rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya. Kampeni zinatarajiwa kuendelezwa leo kote nchini.