1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi Kenya yashindwa kufikia malengo ya usajili

Shisia Wasilwa8 Februari 2022

Tume Huru ya Kusimamia Mipaka na Uchaguzi nchini Kenya, IEBC, kwa mara nyingine tena imeshindwa kutimiza malengo ya kuwasajili wapigakura milioni 4.5 iliokuwa imewakusudia.

https://p.dw.com/p/46fTJ
Kenia | Präsidentschaftswahlen
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Tume hiyo imewasajili wapiga kura milioni moja tu kwenye awamu ya pili ya usajili huo iliyokamilika Jumapili. 

Ilipoanza awamu ya pili yakuwasajili wapigakura kote nchini Kenya tarehe 17 Oktoba mwaka uliopita, Tume ya IEBC ilikuwa na matumaini ya kuwasajili Wakenya wengi, ikizingatiwa kuwa imesalia miezi mitano tu, kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika tarehe tisa Agosti.

Wapiga kura waliosajiliwa ni milioni 1,031, 645.

Hata hivyo, shughuli hiyo ilipokamilika tarehe sita mwezi huu, IEBC haikuwa na la kujivunia baada ya kuwasajili wapiga kura milioni 1,031, 645, kinyume na malengo yake.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, tume hiyo imesema ni wapiga kura 396,163 waliosajaliwa walioomba kuhamishwa kwa vituo vyao vya kupigia kura huku wengine 2269 wakiomba kubadilisha maelezo kwenye nyaraka zao.

Mkuu wa tume ya uchaguzi Kenya IEBC, Wafula Chebukati asema bado wako mbali na malengo ya taifa.
Mkuu wa tume ya uchaguzi Kenya IEBC, Wafula Chebukati asema bado wako mbali na malengo ya taifa.Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Abdul Azim

Awali mwenyekiti wa Tume hiyo, Wafula Chebukati, alionyesha wasiwasi wa kuandikisha wapiga kura milioni 4.5 kama walivyokuwa wamepanga.

"Tuko mbali sana na malengo ya taifa, najua ni safari ndefu. Kwa mujibu wa sheria zetu, kujisajili na kupiga kura, sio lazima, ni haki ya raia wa Kenya, hata hivyo IEBC itaendesha uchaguzi,” Asema Chebukati.

Kwa wapigakura wanaoishi ughaibuni, IEBC iliandikisha wapiga kura 2,959 wapya, huku wengine 2,964 wakiomba kubadilishiwa vituo vyao vya kupigiakura. Wapiga kura 2036 waliomba kubadilishwa kwa maelezo kwenye nyaraka zao.

Sababu za uandikishaji mdogo wa wapiga kura Kenya ni zipi?

Idadi jumla ya waliosajiliwa katika awamu mbili ni milioni 2.5

Tume hiyo ilishindwa kufikia malengo ya kuwasajili wapiga kura milioni sita kwenye awamu hiyo ya kwanza.

Takwimu hizo mpya zinafikisha idadi ya wapiga kura waliosajiliwa kwenye awamu ya pili ya zoezi hilo kuwa milioni 2.5, baada ya Tume kuwasajili wapiga kura milioni 1.5 kwenye awamu ya kwanza.

Sababu mbali mbali zimetolewa kwa uandikishaji mdogo ulioshuhudiwa.

Tume hiyo ilianza zoezi la kuwaandikisha wapiga kura tarehe nne Oktoba hadi tarehe tano Novemba mwaka uliopita ambapo wapigakura wapya milioni moja nukta tano waliandikishwa.

Punde tu baada ya zoezi la kujiandikisha litakapokamilika, ukaguzi wa daftari la wapigakura utafanyika kisha walioandikishwa kuthibitishwa.

Wakenya wanaoishi Uingereza, Marekani, Sudan Kusini, Falme za Kiarabu na Ujerumani pia walishiriki zoezi la kujiandikisha. IEBC haijatoa sababu za uandikishaji huo mdogo.