1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wapiga kura leo

20 Desemba 2023

Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo muda mfupi kutoka sasa wanajiandaa kupiga kura kumchagua rais, wabunge, magavana wa mikoa pamoja na madiwani baada ya muda wa kampeni ya mwezi mmoja kukamilika siku ya Jumatatu.

https://p.dw.com/p/4aMtm
Uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Mashine mpya ambayo itatumika wakati wa zoezi la uchaguzi Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi nchini humo, watu milioni 40 kati ya idadi jumla ya Wakongomani milioni 100 wamesajiliwa kama wapiga kura.

Rais Felix Tshisekedi mwenye umri wa miaka 60 anawania muhula mwingine wa miaka mitano.

Kiongozi huyo anakabiliana na wanasiasa kadhaa wa upinzani akiwemo mfanyabishara mashuhuri Moise Katumbi, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Daktari Denis Mukwege na Martin Fayulu, mgombea aliyeshindwa na Tshisekedi katika uchaguzi wa mwaka 2018.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini humo CENI Denis Kadima amesema hana uhakika juu ya iwapo vituo vyote vya kupigia kura vitafunguliwa kwa wakati, lakini amehakikisha kuwa watu wote wenye haki ya kupiga kura watatekeleza haki yao, hata ikimaanisha zoezi hilo kwenda hadi siku ya pili.

Kadima amebainisha kuwa CENI imerikodi mashambulizi 3,244 ya wadukuzi kwenye mtandao wake siku ya Jumatatu pekee, na kubainisha kuwa kuna wahalifu wanaojaribu kuvunja mfumo wa tume hiyo, na kuongeza kuwa wamefanikiwa kuwazuia na kuimarisha mfumo huo.

Kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi, matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa mnamo Disemba 31.