1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Qin aukwepa wito wa Afrika kuwa na kiti cha kudumu UN

12 Januari 2023

Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang amejizuia kuzungumzia wito mpya uliotolewa na Umoja wa Afrika kutaka uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wakati wa ziara yake nchini Ethiopia.

https://p.dw.com/p/4M5Sh
Chinesischer Außenminister Qin Gang in Äthiopien
Picha: Fana Broadcasting Corporate

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa makao makuu ya Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika, Qin badala yake amesisitiza kuhusu umuhimu wa ushirikiano kati ya China na Afrika katika masuala ya usalama na maendeleo ya kiuchumi. Kituo hicho kilichojengwa kwa udhamini wa China, kiko kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

China yataka sauti zaidi ya Afrika kimataifa

Katika taarifa iliyotolewa mapema Alhamisi asubuhi, wizara ya mambo ya nje ya China imemnukuu Qin akisema nchi yake inaunga mkono uwakilishi na sauti zaidi wa Umoja wa Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa, lakini hakuzungumzia moja kwa moja uwakilishi wa kudumu.

Mwenyekiti wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, ameuambia mkutano wa pamoja wa waandishi habari na Qin kwamba hatua ya Afrika kukosa uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni suala muhimu na la kipaumbele ikizingatiwa kwamba masuala mengi katika ajenda ya baraza hilo yanazihusu nchi za Kiafrika.

Moussa Faki Afrikanische Union
Mwenyekiti wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki MahamatPicha: Michael Kappeler/picture alliance/dpa

Mahamat, amesema haikubaliki kwamba wengine wanaamua kwa niaba ya wengine. Amesema hiyo sio haki na kwamba wanahitaji utaratibu mpya katika ngazi ya kimataifa ambao utaheshimu maslahi ya wengine. China ni miongoni mwa nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

China yakanusha kuhusu mtego wa madeni Afrika

Ama kwa upande mwingine, Qin amekanusha madai kwamba China inaanzisha kile kinachoitwa ''mtego wa madeni barani Afrika. Amesema katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Afrika zimekuwa zikifanya kazi kwa bidii kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii, lakini uhaba wa fedha umekuwa kikwazo kikubwa kwa ustawi wake.

''China imejizatiti kuisaidia Afrika kupunguza mzigo wa madeni na inashiriki kikamilifu katika mpango wa msamaha wa madeni, wa kundi la nchi zilizoendelea na zinazostawi kiuchumi duniani, G20. Afrika inahitaji mshikamano na ushirikiano, na sio kuzuia ushindani,'' alifafanua Qin.

Annalena Baerbock in Äthiopien
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Catherine Colonna Picha: Florian Gärtner/imago images/photothek

Qin ambaye aliteuliwa mwezi Desemba kushika nafasi ya waziri wa mambo ya nje, yuko katika ziara yake ya kwanza nchi za nje tangu ashike wadhifa huo na ameanza na ziara ya wiki nzima kwenye nchi za Afrika, ikiwemo Ethiopia, Gabon, Angola, Benin na Misri. China imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye miundombinu katika nchi za Afrika, ikiwemo katika barabara, reli na hospitali.

Soma zaidi: Mawaziri wa Ujerumani na Ufaransa waizuru Ethiopia

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock na mwenzake wa Ufaransa, Catherine Colonna wanaizuru pia Ethiopia. Wanadiplomasia hao tayari wameshakutana na Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde pamoja na Waziri Mkuu, Abiy Ahmed. Siku ya Ijumaa Baerbock na Colonna watakutana na Mwenyekiti wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat.

(AP, AFP)