1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Mawaziri wa Ujerumani na Ufaransa waizuri Ethiopia

12 Januari 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock na mwenzake wa Ufaransa, Catherine Colonna wamewasili mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa ziara ya siku mbili.

https://p.dw.com/p/4M3QI
Außenministerin Baerbock in Äthiopien
Picha: Michael Kappeler/dpa

Wanadiplomasia hao wanaizuru Ethiopia wakati ambapo nchi hiyo inakabiliana na mzozo wa njaa unaosababishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Mawaziri hao watakutana na Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde, na kuunga mkono makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka uliopita. Katika ziara hiyo, Baerbock na Colonna wanatarajiwa pia kukutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, Waziri wa Mambo ya Nje, Demeke Mekonnen na Waziri wa Sheria, Gedion Timothewos.

Umoja wa Ulaya waunga mkono shughuli za kiutu

Wanadioplomasia hao pia watalitembelea ghala la nafaka la Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, lililoko nje ya mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, ambako nafaka zinazotoka Ukraine zinahifadhiwa.

Ziara ya mawaziri hao zinafanyika wakati ambapo serikali ya Ethiopia na chama cha Watu wa Ukombozi wa Tigray, TPLF wanautekeleza mpango wa amani uliosainiwa mwezi Novemba mwaka uliopita, kuvimaliza vita vilivyodumu kwa miaka miwili. Januari 5, Waziri Colonna alisema kuwa ziara yao itasisitiza uungaji mkono mkataba huo wa amani uliosimamiwa na Umoja wa Afrika.

Äthiopien Tigray | Waffenübergabe der Rebellen an Armee
Waasi wa Tigray wameanza kusalimisha silaha za kivita kwa jeshi la EthiopiaPicha: Ethiopian Broadcasting Corporation

Mengistu Assefa, mchambuzi wa masuala ya siasa aliyeko mjini Addis Ababa anasema wanadiplomasia hao wanataka kuhakikisha kwamba mpango huo unaleta amani ya kudumu nchini Ethiopia. Mengistu anasema uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Ethiopia, ulipungua baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Tigray vilipoibuka.

Ethiopia ilikosolewa na Umoja wa Ulaya 

''Umoja wa Ulaya uliikosoa serikali ya Ethiopia, hasa kuhusu namna inavyovishughulikia vita hivyo, kutokana na taarifa za ukiukaji wa sheria za haki za binaadamu. Hiyo ilisababisha kupunguzwa kwa msaada wa maendeleo kwa serikali ya Ethiopia,'' alifafanua Mengistu.

Umoja wa Ulaya ni moja kati ya wafadhili wakubwa wa Umoja wa Afrika. Hata hivyo, Ethiopia haikuualika Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya amani, ambayo yalifanikisha kusainiwa kwa makubaliano mjini Pretoria, Afrika Kusini. Kwa mujibu wa baadhi ya waangalizi, uamuzi huo ulisababisha kutoridhika kwa umoja huo wenye makao yake mjini Brussels.

Tigray I Lastwagen des Internationalen Komitees vom Roten Kreuz (IKRK)
Msafara wa malori ya Kamati ya Kimtaifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC yakipeleka vifaa vya matibabu kuelekea MekellePicha: International Committee of the Red Cross/Handout/REUTERS

Annette Weber, mwakilishi maalum wa Umoja wa Ulaya katika Pembe ya Afrika amesema uhusiano wote kati ya nchi wanachama wa umoja huo na Ethiopia ulikuwa mgumu wakati wa mzozo wa Tigray katika miaka miwili iliyopita.

''Lakini nadhani uhusiano na Ujerumani umekuwa wa muda mrefu sana, uhusiano wa kuaminika ambao umekuwa mkubwa. Na kile tunachokiona sasa hivi ni kuunyoosha uhusiano, baada ya makubaliano ya amani kusainiwa, alisema Weber.''

Baerbock na Colonna kukutana na viongozi wa Umoja wa Afrika

Aidha, msemaji wa Umoja wa Afrika katika ofisi ya mambo ya nje mjini Berlin, amesema mawaziri hao wawili pia watafanya mazungumzo na viongozi wa Umoja wa Afrika. Mkutano kati ya mawaziri hao wa Ujerumani na Ufaransa na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat umepangwa kufanyika kesho Ijumaa.

Ziara ya Baerbock na Colonna inafanyika siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Qin Gang kuanza ziara ya wiki nzima kwenye mataifa ya Afrika, ikiwemo Ethiopia. Kabla ya ziara ya Qin, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, James Claverly aliizuru pia Ethiopia, ambako alishuhudia utoaji wa misaada ya kiutu.

(DW)