1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Kiongozi wa Hamas kuzikwa Qatar

2 Agosti 2024

Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh aliyeuawa nchini Iran anazikwa hii leo huko Doha, Qatar. Rais Joe Biden wa Marekani licha ya kuahidi kuendelea kuilinda Israel, ameonyesha wasiwasi wake kuhusiana na mauaji hayo.

https://p.dw.com/p/4j2CQ
Iran imeapa kulipiza kisasi kifo cha Ismail Haniyeh
Ismail HAniyeh, kiongozi wa kundi la Hamas alyieuawa nchini Iran anazikwa hii leo huko Doha, QatarPicha: IMAGO/NurPhoto

Mwili wa Ismail Haniyeh uliwasili tangu jana Alhamisi katika mji mkuu wa Qatar, Doha tayari kwa mazishi na baadhi ya picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha mkewe Amal akiomboleza kwenye jeneza la mumewe kabla ya kuzikwa.

"Wewe ni msaada wangu kwenye maisha ya sasa na ya baadae. Kipenzi changu. Wasalimie mashahidi wa Gaza, wasalimie viongozi wote na waislamu wote.... Mpendwa wangu, Mungu akupunguzie adhabu..... kichwa cha moyo wangu..... Asante Mungu," aliomboleza Amal.

Kulingana na taarifa ya Hamas, kiongozi wake huyo atazikwa katika makaburi yaliyoko Lusali baada ya swala ya Ijumaa itakayofanyika kwenye msikiti wa Imam Mohammad Abdul Wahhab, ambao ni mkubwa kabisa huko Qatar na waombolezaji walianza kumiminika kwenye msikiti huo tangu mapema leo.

Ismail Haniyeh amekuwa akiishi mjini Doha pamoja na wajumbe wengine wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, lakini alikutwa na mauti siku ya Jumatano akiwa mjini Tehran Iran kufuatia shambulizi la anga ambalo pia lilimuua mlinzi wake baada ya kutoka kwenye sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Iran. Kiongozi wa juu nchini humo Ayatollah Ali Khamenei aliahidi kulipiza kisasi kwa damu hiyo iliyomwagika kwenye ardhi yake.

Kundi hilo la Kipalestina, linaishutumu Israel kwa mauaji hayo yaliyowashtusha na yaliyoongeza mashaka kwamba huenda Ukanda mzima wa Mashariki ya Kati ukaingia kwenye vita kamili. 

Soma pia: Je Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh ni nani?

Israel ilisema ni lazima imuue Haniyeh na viongozi wengine wa Hamas baada ya kundi hilo kuishambulia Israel Oktoba 7, 2023.

Biden aonyesha wasiwasi juu ya kifo cha Haniyeh

Rais Joe Biden ameonyesha dhahiri wasiwasi wake baada ya kifo cha Haniyeh, akisema hakitasaidia chochote katika kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza na badala yake kimeongeza mafuta kwenye moto uliokolea. Biden amekiri kwamba ana wasiwasi mkubwa.

Marekani Washington 2024 | Rais wa MArekani Biden na Waziri Mkuu wa Israel, Netanyahu
Rais Joe Biden akiwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wakijadili jambo mjini Washington. Biden amewasiliana na Netanyahu akimsisitizia juu ya kusitisha mapiganoPicha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Amesema, amezungumza moja kwa moja kwa nijia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mapema jana Alhamisi na kumwambia wanatakiwa kuchukua hatua sasa za kusitisha vita.

Hadi sasa, Israel haijathibitisha kuhusika na mauaji hayo ya Haniyeh.

Soma pia: Khamenei aapa 'adhabu kali'' kwa Israel baada ya mauaji ya Haniyeh

Lakini pamoja na wasiwasi huo, Biden ameendelea kusisitiza kwamba Marekani itaendelea kuwajibika kuilinda Israel dhidi ya vitisho vyote kutokea Iran. Biden aliungana na makamu wake Kamala Harris kwenye mazungumzo hayo, imesema taarifa ya White House.

Na nchini Australia, serikali ya taifa hilo imelishutumu jeshi la Israel, IDF kwa kushindwa vibaya kuzuia vifo vya wafanyakazi wa misaada. Waziri wa Mambo ya Nje, Penny Wong ametolea mfano shambulizi ya Israel la mwezi Aprili lililowaua wafanyakazi saba wa shirika la misaada la World Central Kitchen huko Gaza hatua iliyoibua ukosoaji mkubwa na uchunguzi unaonyesha mauaji hayo yalisababishwa na makosa ya IDF kuanzia kushindwa kuwatambua hadi makosa katika kufanya maamuzi.

Soma pia: Israel yaendeleza mashambulizi Gaza licha ya ukosoaji wa Marekani