1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khamenei: Adhabu kali kwa Israel baada ya mauaji ya Haniyah

31 Julai 2024

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameapa kutoa kile alichokiita adhabu kali kwa Israeli baada ya mauaji ya kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran.

https://p.dw.com/p/4ix2K
Iran | Ismail Haniyeh
Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh aliyeuwawa nchini IranPicha: Iran's Presidency/WANA/REUTERS

Katika taarifa iliyorushwa na shirika la habari la IRNA, Khamenei amesema kwa hatua hiyo, nikinukuu, ''mhalifu na utawala wa kigaidi wa Kizayuni'', umejitayarishia msingi wa adhabu kali.

Khamenei ameongeza kuwa wanaona ni jukumu lao kulipiza kisasi kwasababu Haniyeh ameuawa katika ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

"Tunazingatia sana tukio hili. Tunapinga na kulaani vikali kitendo cha mauaji. Tuna wasiwasi mkubwa kwamba tukio hili linaweza kusababisha kuongezeka kwa machafuko katika eneo hili. China daima imekuwa ikitetea utatuzi wa migogoro ya kikanda kwa njia ya mazungumzo," ilisema China kupitia msemaji wake wa wizara ya mambo ya nje Lin Jian.

Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh auwawa Iran

Kundi la Hamas limedai kuwa Haniyeh aliuawa kwenye makazi yake mjini Tehran katika shambulio la anga la Israel baada ya kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa kiongozi  mpya wa Iran.

Hata hivyo Israel haijatoa tamko kuhusu tukio hilo.