1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin awasili mjini Tehran kwa mazungumzo na rais wa Iran

1 Novemba 2017

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewasili katika mji mkuu wa Iran, Tehran kwa ziara inayochukuliwa na uongozi wa Jamuhuri hiyo ya Kiislam kama upinzani wa wazi dhidi ya sera ya nchi za nje ya Marekani.

https://p.dw.com/p/2mrNT
Iran Wladimir Putin & Hassan Rohani in Teheran
Picha: Reuters/Sputnik/Alexei Druzhinin/Kremlin

Rais Putin atakutana na mwenzake wa Iran, Hassan Rouhani, ambaye anasubiri tamko la kuunga mkono makubaliano ya mpango wa nyuklia wa Iran ya mwaka 2015, yanayohusiana na Iran kupunguza mpango wake wa nyuklia ili iondolewe vikwazo vya kimataifa. Mkutano huo wa mjini Tehran unafanyika wakati ambapo mpango wa nyuklia wa Iran unatishiwa na Rais wa Marekani Donald Trump kwamba hatoyathibitisha makubaliano hayo ya mwaka 2015. Trump ameyakosoa vikali makubaliano hayo na ametishia kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi.

Marekani inaituhumu Iran kwa kujaribu kutengeneza bomu la nyuklia lakini rais wa nchi hiyo Donald Trump pia hajaelezea iwapo Marekani itazingatia au kuyafutilia mbali makubaliano ya mwaka 2015 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Iran Hassan Rouhani
Rais wa Iran Hassan RuohaniPicha: picture alliance/AP Photo/Iranian Presidency Office

Rais wa Iran Hassan Rouhani ambaye amepangiwa kukutana na Rais wa Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev, alitarajiwa kujadili uimarishaji wa mahusiano ya kiuchumi na viongozi hao wawili. Iran inaamini kuwa mkutano huu utaonyesha kuwa ushirikiano wa kikanda hauhitaji idhini ya Marekani. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Ebrahim Rahimpur alisema Jumanne kuwa hakuna anaezingatia vita vya maneno vya Marekani kwa sasa. Ziara ya Putin pia inatarajiwa kuhusisha majadiliano juu ya ushirikiano wa Iran na Urusi katika mgogoro unaoendelea nchini Syria.

Nchi hizo ni washirika wa rais wa Syria Bashar al Assad na zinapambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS na zote zinataka uchaguzi wa Syria ufanyike na pia umjumuishe rais Bashar al Assad.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran ameliambia shirika la habari la Iran kwamba kwa upande wa uchumi, mkutano huo wa mjini Tehran utaangalia hasa fursa mpya za kibiashara na pia utaangazia juu ya upatikanaji wa masoko ya Ulaya kupitia Bahari nyeusi, wakati Urusi na Azerbaijan zinaweza kuyafikia masoko ya Kiarabu kupitia eneo la Ghuba.

Russland Präsident Wladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir putinPicha: picture-alliance/dpa/TASS/M. Metze

Mazungumzo ya mjini Tehran yatazingatia mambo ya kikanda, pamoja na masuala ya ugaidi na usalama. Masuala mengine yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo ni pamoja na ushirikiano katika bahari ya Caspian,reli na miradi ya barabara. Rais wa Urusi Vladmir Putin aliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mehrabad kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo wa siku moja.

Ni ziara yake ya tatu nchini Iran baada ya awali kuizuru nchi hiyo mnamo mwaka 2015 na pia mwaka 2007.  Putin atakutana pia na kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, mwenye maamuzi ya mwisho juu ya mambo yote ya kiserikali. Nchi hizo mbili zina maslahi mengi yanayofanana.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga