1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin alipongeza jeshi na vyombo vya usalama

Josephat Charo
27 Juni 2023

Rais wa Urusi Vladimir Putin leo amelenga kuyaunganisha majeshi na vyombo vya usalama akiwaambia wamefanikiwa kuepusha nchi kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/4T7xL
Russland l russische Präsident Putin spricht auf dem Kathedralenplatz am Kreml
Picha: Sputnik/Sergei Guneev/Pool via REUTERS

Rais Putin alilipongeza jeshi na vyombo vya usalama kwa kuepusha vita vya wenyewe kwa wenyewe Urusi kwa kuchukua hatua ya kuupinga uasi wa kijeshi ulioongozwa na kiongoni wa kampuni ya ulinzi ya wapiganaji mamluki ya Wagner Yevgevy Progozhin. Akiwahutubia wanajeshi na maafisa wa usalama katika ikulu ya Kremlin, Putin aliisifu hatua yao wakati wa uasi wa Wagner, akisema walifanikiwa kikamilifu kuepusha vita nchini.

Putin alisema, "Mumeulinda utawala wa kikatiba, maisha, usalama na uhuru wa raia wetu. Mumeiokoa nchi yetu, mumeepusha machafuko na kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mlichukua hatua ya wazi ya umoja na utulivu wakati wa kipini kigumu."

Soma zaidi: Urusi yasema Prigozhin hatashtakiwa

Putin ametangaza kwamba jeshi na Warusi hawaungi mkono uasi huo lakini akajiepusha kumtaja Prigozhin kwa jina lake. Amesisitiza kwamba vikosi vya Urusi havijaondolewa katika uwanja wa vita nchini Ukraine kuushughuikia uasi huo. Urusi imefutilia mbali mashitaka dhidi ya Prigozhin na wengine walioshiriki uasi huo uliodumu muda mfupi. Msamaha huo uliotangazwa ni tukio la hivi karibuni la kushangaza miongoni mwa matukio yaliyoshuhudiwa siku chache zilizopita ambayo yamesababisha kitisho kikubwa kwa madaraka ya Putin tangu vita vya Ukraine vilpozuka.

Mamlaka ya Putin yako imara

Rais Putin pia amesema kampuni ya Wagner ilifadhiliwa kikamilifu na Urusi, ambapo ilitumia rubi bilioni 86.26, sawa na dola bilioni 1.01 kati ya Mei 2022 na Mei 2023. Aidha amesema kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin, aliyeoongoza uasi Jumamosi iliyopita, alipata faida ya fedha kiwango kama hicho kutokana biashara yake ya chakula. Putin amesema Prigozhin atachunguzwa.

Russland Jewgeni Prigoschin Statement in Rostow-am-Don
Kiongozi wa Wagner PrigozhinPicha: Press service of "Concord"/REUTERS

Huku Urusi ikitangaza mipango ya kuwapokonya silaha wapiganaji mamluki wa Wagner, rais Putin na wafuasi wake wamesisitiza kwamba utawala wake haujadhoofishwa na uasi huo unaoonekana kuwa kitisho kikubwa kwa utawala wa Kremlin tangu Putin alipoingia madarakani. Alipoulizwa ikiwa mdaraka ya Putin yamepungua kufuatia uasi wa Wagner na hatua yao ya kuyateka makao makuu ya jeshi na kuelekea mjini Moscow na kuitungua ndege ya kivita ya jeshi, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema hawakubaliani kabisa na hoja hiyo.

Soma zaidi: Putin azishutumu Ukraine, Magharibi kuchochea mauaji Urusi

Wakati haya yakiarifiwa shirika la habari la serikali ya Belarus BELTA limemnukuu rais wa Belarus Alexander Lukaschenko akithibitisha kuwa muasisi wa kampuni ya Wagner Prigozhin yuko Belarus. Lukaschenko pia amesema waziri wa ulinzi wa Belarus, Viktor Khrennikov amemwambia hangejali kuwa na kitengo kama Wagner katika jeshi la Belarus. Lukaschenko amemuagiza waziri wake wa ulinzi Khrennikov afanye mazungumzo na Prigozhin kuhusu suala hilo.

(afpe, reuters)