1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasema Prigozhin hatashitakiwa

27 Juni 2023

Urusi imetangaza kuachana na uchunguzi juu ya uasi wa kutumia silaha ulioongozwa na mkuu wa kundi la wapiganaji la Wagner, Yevgeny Prigozhin, ikisema hakutakuwa na mashtaka yoyote dhidi yake au washiriki wengine wowote.

https://p.dw.com/p/4T6kj
Russland Jewgeni Prigoschin Statement in Rostow-am-Don
Picha: Press service of "Concord"/REUTERS

Shirika la Usalama la Urusi (FSB) limesema uchunguzi wake ulibaini kuwa  wale waliohusika katika uasi walisitisha maelekezo ya kufanya uhalifu huo.

Hii ni baada ya mwishoni mwa juma serikali kutoa ahadi ya kutomshitaki Prigozhin na wapiganaji wake baada ya kusitisha uasi wa Jumamosi iliyopita, ingawa Rais Vladimir Putin aliwapaichka wapiganaji hao jina la waasi.

Shitaka la kuanzisha uasi wa kutumia silaha lina adhabu ya hadi miaka 20 jela.

Ukraine: Working trip of the President of Ukraine to Donetsk region
Rais Volodymyr Zelensky (katikati) akiwatembelea wanajeshi kwenye uwanja wa mapambano jimbo la Donetsk.Picha: POU/ROPI/picture alliance

Hadi kufikia Jumanne (Juni 27) mahali alipo Prigozhin palikuwa pamesalia kuwa siri.

Serikali ya Urusi ilisema kiongozi huyo wa kundi la Wagner angelihamishwa taifa jirani la Belarus, ingawa si yeye  wala mamlaka ya Belarus waliothibitisha hilo.

Pongezi za Rais Zelensky kwa wapiganaji

Katika uwanja wa mapambano, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alisema mapambano ya majuma kadhaa yenye lengo la kuyadhibiti tena maeneo yaliyochukuliwa na Urusi yanaendelea kwa mafanikio.

"Leo hii katika maeneo ya mapambano, mikoa ya Donetsk na Zaporizhzhia, wanajeshi wetu wako vyema katika maeneo ya makabiliano. Kwa hivyo nina furaha. Nawatakia wapambanaji siku nyingine zaidi kama hizi. Hongereni sana!" Alisema kiongozi huyo wakati akiwa kwenye treni kutokea mstari wa mbele wa mapambano.

Urusi yawanyonga watu 77

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa,  Urusi imewanyonga watu 77 waliokuwa wakishikiliwa kiholela wakati wa vita vyake nchini Ukraine.

Tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake Februari 2022, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kufuatilia Haki za Kibinadamu nchini Ukraine umerekodi visa 864 vya kuwekwa kizuizini kiholela vinavyofanywa na Urusi, vingi vikiwa vya utoeshwaji wa watu.

Kiongozi wa ujumbe huo, Matilda Bogner alisema kati ya hao 77 wanaume walikuwa 72 na wanawake watano, ambapo wafungwa wawili wa kiume walikufa kutokana na mateso na kunyimwa huduma za matibabu.

Soma zaidi:Urusi yahofiwa kutoongeza makubaliano ya ngano ya Ukraine

Matokeo ya ripoti hiyo yalitokana na mahojiano 1,136 na waathiriwa, mashahidi na wengine, pamoja na kutembelea maeneo 274 ya vizuizini yanayoendeshwa na mamlaka ya Ukraine.

Kwa ujumla, ripoti hiyo ilinakili zaidi ya kesi 900 za kuwekwa kizuizini kiholela kwa raia, wakiwemo watoto, na wazee.

Vyanzo: AFP/DPA