1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baadhi ya wakimbizi wameondoka Belarus na kurejea Iraq

Zainab Aziz Mhariri: Grace Kabogo
19 Novemba 2021

Hali ya wasiwasi katika mpaka wa mashariki wa Umoja wa Ulaya inaweza kufikia hatua ya sintofahamu licha ya baadhi ya wahamiaji kuondoka na Belarus kuanza kuzifunga kambi za wahamiaji kwenye mpaka wake,

https://p.dw.com/p/43Fx6
Irak Erbil Airport | Ankunft Migranten aus Belarus
Picha: Safin Hamed/AFP/Getty Images

Kulingana na msemaji wa walinzi wa mpakani wa Poland, Anna Michalska maafisa wa Belarus wanawasaidia wahamiaji hao kuvuka mpaka na kuingia nchini mwake mara baada ya Belarus kuzifunga kambi zilizo karibu na mji wa mpakani wa Bruzgi. Michalska amesema kundi la karibu wahamiaji 500 walijaribu kuvuka mpaka hapo jana siku ya Alhamisi baada ya kambi hizo kufungwa upande wa Belarus.

Matarajio ya umati wa wahamiaji waliokusanyika katika mpaka wa Belarus na Poland yametatizika, huku baadhi yao wakionekana kukata tamaa ya kuvuka mpaka huo na kuingia katika Umoja wa Ulaya, lakini wakati huo huo wahamiaji zaidi wanaendelea kujitokeza katika mpaka huo. Viongozi wa dunia nao bado wanafanya mazungumzo kutafuta njia za kuumaliza mgogoro huo.

Mamia ya wakimbizi wamerejea nchini Iraq baada ya kuona kuwa uwezekano wa wao kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya ni mdogo..

Wakimbizi waliorejea nchini Iraq kutoka Belarus
Wakimbizi waliorejea nchini Iraq kutoka BelarusPicha: AZAD LASHKARI/REUTERS

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko analaumiwa kwa sakata hilo la wahamiaji katika mpaka baina ya nchi yake na Poland anahusishwa na kuwatia moyo maelfu ya watu kutoka nchi zinazokabiliwa na vita kuja Belarus na kuwaahidi kuwa watapata maisha bora katika nchi za Ulaya. Umoja wa Ulaya unadai kuwa Lukashenko aliwaruhusu wahamiaji hao kuelekea upande wa mashariki kwenye mpaka na Poland yote hayo ikiwa ni kulipiza kisasi kwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya utawala wake. Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema mbinu za Belarus za kuwatumia watu vibaya ni hatari.

Kushoto: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Kulia: Rais wa Belarus Alexandar Lukashenko.
Kushoto: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Kulia: Rais wa Belarus Alexandar Lukashenko.

Siku ya Jumatano, kiongozi wa Belarus alipozungumza kwa simu na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alikubali kwamba atashiriki kwenye mazungumzo na Umoja wa Ulaya kuhusu mgogoro huo. Ingawa mazungumzo hayo hayakugusia matarajio ya Poland kufungua mpaka wake wakati wowote hivi karibuni, lakini si haba yamefungua njia ya kufikishwa misaada katika eneo la mpaka. Shughuli za kidiplomasia zinaendelea katika jitihada za kuutatua msukosuko ambao unaweza kusababisha mgogoro wa kibinadamu.

Vyanzo:/RTRE/DPA