1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Picha za Abyei 'zaiumbua' Sudan ya Kaskazini

26 Mei 2011

Picha mpya zilizotolewa leo zinaonyesha wanajeshi wa Sudan Kaskazni waliandaa uporaji mali katika mji wa mpakani wa Abyei unaogombewa na Kaskazini na Kusini baada ya majeshi ya Kaskazini kuuteka mji huo wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/RQ8m
Ramani ya Sudan ikionesha Kusini, Kaskazini na jimbo linalogombewa la Abyei

Shirika la Marekani linalojulikana kama Enough Project, ambalo limepokea picha hizo, linasema picha zinaelekea kuonyesha wanajeshi wa Kaskazini wakisaidiwa na wanamgambo, wakijaza vyakula na bidhaa nyengine kwenye magari.

Shirika hilo limesema picha hizo zinatoa ushahidi juu ya visa vya uporaji mali vilivyotokea Abyei.

Picha nyengine zinaonyesha nyumba zikiwashwa moto na watu wenye silaha wakiwa katika mavazi ya kiraia wakirandaranda mjini humo.

Kutekwa kwa mji wa Abyei na majeshi ya Kaskazini, kukisalia wiki chache kabla ya Sudan Kusini kuwa huru, kumelaaniwa ana madola makuu duniani, kukitajwa kuwa ni kitisho kwa amani kati ya Kaskazini na Kusini.

Lakini serikali ya Rais Omar Hassan al-Bashir imesisitiza kwamba Abyei ni sehemu ya Kaskazini na kwamba itabakia hivyo hadi hapo wakaazi wake watakapoamua vyenginevyo.

Umoja wa Afrika yasisitiza inao uwezo wa kutafuta suluhu ya Libya

Ndege za NATO zinazoshambuliwa Libya
Ndege za NATO zinazoshambuliwa LibyaPicha: Picture-Alliance/dpa

Umoja wa Afrika umesema bado unataka kutafuta suluhisho la kisiasa la mzozo unaoendelea nchini Libya, licha ya kuimarishwa kwa mashambulizi ya anga ya ndege za Jumuiya ya Kujihami ya NATO dhidi ya utawala wa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Jean Ping, amesema ni suluhisho la kisiasa pekee litakaloleta amani ya kudumu pamoja na matumaini ya umma wa Libya.

Ping aliyasema hayo katika mkutano wa Umoja wa Afrika ulioitishwa mjini Addis Ababa kuzungumzia mgogoro huo na kuhudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon. Mkutano huo pia ulijadili juu ya matukio nchini Cote d´Ivoire na Sudan.

Kwa upande mwengine, jana mjini London Rais Barack Obama wa Marekani, ambaye yuko ziarani barani Ulaya alimuonya Kanali Gaddafi akisema shinikizo dhidi yake litaendelea.

Matamshi haya ya Rais Obama yamekuja wakati ndege za NATO zikiendelea kuuhujumu mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Munyagishari akamatwa

Wakimbizi wa Kongo
Wakimbizi wa Kongo

Mahakama maalumu ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda, ICTR, yenye makao yake mjini Arusha, nchini Tanzania, imesema Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imemkamata, kiongozi wa zamani wa kundi la waasi, Bernard Munyagishari.

Mshukiwa huyo amekuwa akitafutwa kujibu mashtaka kwa kuwa miongoni mwa watu waliopanga mauaji ya halaiki na kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwa ni pamoja na ubakaji.

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICTR, Hassan Bubacar Jallow, alitangaza jana kukamatwa kwa Munyagishari huko Kachaga, katika jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Kongo. Munyagishari alikuwa kiongozi wa kundi la waasi la Interahamwe huko Gisenyi.

Manmohan Singh kuwasili Tanzania

Waziri Mkuu wa India, Manmohan Singh
Waziri Mkuu wa India, Manmohan SinghPicha: UNI

Waziri Mkuu wa India, Manmohan Singh, leo anawasili nchini Tanzania kwa ziara ya kiserikali.

Singh anatokea Addis Ababa, Ethiopia, ambako alishiriki katika mkutano wa kilele kati ya India na nchi za Kiafrika.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zenye uhusiano wa karibu na India. Mazungumzo kati ya Waziri Mkuu Singh na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete, yanatarajiwa kutuwama katika masuala ya kuimarisha biashara kati ya nchi zao mbili.

Nigeria yamuunga mkono Blatter uraisi wa FIFA

Rais wa FIFA Sepp Blatter
Rais wa FIFA Sepp BlatterPicha: dapd

Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) linasema litamuunga mkono Sepp Blatter kuliongoza Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) katika uchaguzi uliopangwa kufanyika wiki ijayo.

NFF imesema jana limeamua kumuunga mkono Blatter kwa kuahidi kupambana na rushwa na kuufanya uongozi wa mchezo wa kandanda kuwa wazi zaidi.

Uamuzi wa Nigeria ulichukuliwa muda mfupi kabla mpinzani wa Blatter, Mohammed bin Hammam wa Qatar, kuanza kuchunguzwa na kamati ya maadili ya FIFA kwa kutuhumiwa kutoa rushwa wakati wa kampeni yake.

Blatter mwenye umri wa miaka 75 na ambaye amekuwa akiiongoza FIFA kwa miaka 13, ameungwa mkono na Shirikisho la Dimba Afrika (CAF) na mashirikisho mengine matano barani humo, hivyo kuashiria kufifia kwa uungaji mkono wa Hammam katika bara anakoaminiwa kuwa na ufuasi mkubwa.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman

Mhariri: Josephat Charo