1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pazia la kampeni za uchaguzi wa rais lafunguliwa Brazil

17 Agosti 2022

Kampeni za uchaguzi wa rais nchini Brazil utakaofanyika mwanzoni mwa Oktoba zimefunguliwa kwa wagombea wawili vigogo kushambuliana kwa maneno makali na vijembe.

https://p.dw.com/p/4Fd66
Brasilien Wahl Lula da Silva in Sao Bernardo do Campo
Lula da Silva akifungua kampeni za uchaguzi wa rais Picha: Andre Penner/AP Photo/picture alliance

Kampeni hizo za uchaguzi nchini Brazil zimeanza kwa mshikemshike baada ya wagombea wawili vinara kufungua pazia la kuomba kura kwa hotuba zilizojaa ubabe wa maneno jukwaani na kila mmoja akimshambulia mwengine tena kwa matamshi makali.

Luiz Inacio Lula da Silva ambaye aliitawala Brazil kwa mihula miwili kati ya mwaka 2003 hadi 2010, alifungua kampeni yake ya kuwania tena wadhifa huo kwa mkutano kwenye kiwanda kimoja cha kuunda magari nje kidogo ya mji wa Sao Paulo.

Aliutumia mkutano wake wa kwanza kumpiga vijembe rais aliye madarakani Jair Bolsonaro akimtaja kuwa mwanasiasa "muongo na mwenye hadaa" na kwa hivyo hakuna njia itakayomrejesha madarakani.

Ameutuhumu utawala wa Bolsonaro kwa kuirejesha Brazil katika baa la njaa, mfumuko mkubwa wa bei huku sera zake za mrengo wa kulia zinazopigia upatu umiliki binafsi wa bunduki zimeongeza kitisho kwa usalama wa taifa.

"Ninataka nikueleze, wewe rais katili: hatutaki serikali inayosambaza silaha, tunataka serikali inayosambaza vitabu, hatutaki serikai inayopalilia chuki tunataka serikali inayohimiza upendo" amesema Lula.

Bolsonaro ajibu mapigo wakati wa mkutano wa kwanza 

Brasilien Wahl Bolsonaro in Juiz de Fora
Rais Jair Bolsonaro wakati wa mkutano wake wa kwanza wa kampeni Picha: Silvia Izquierdo/AP Photo/picture alliance

Yumkini haikuwa Lula da Silva pekee aliyeonesha kipawa cha kutumia maneno makali jukwaani. Bolsonaro naye alipopanda jukwaani huko katika mji wa Juiz de Fora alimshambulia mpinzani wake kwa maneno ya stizahi akiwakumbusha wapigakura kuwa Lula amewahi kutiwa hatiani kwa makosa ya rushwa na kwa hivyo hafai kuchaguliwa tena kuiongoza Brazil.

Hata hivyo ukweli ni kwamba licha ya Lula kutiwa hatiani kwa kesi ya rushwa na kufungwa jela kwa miaka kadhaa, mwezi Machi mwaka jana mahakama ya juu nchini Brazil ilifuta hukumu dhidi yake na kumfungulia njia ya kurejea katika ulingo wa siasa.

Mbali ya kumlenga mpinzani wake, Bolsonaro pia alitetea rikodi yake madarakani akisema serikali yake imefanya kazi kubwa tangu alipochaguliwa mwaka 2018.

"Hakuna ulinganifu kwa miaka minne ya serikali yangu na minne ya yule mwingine aliyewahi kuwa rais, sisi tumeonesha mfano wa uzalendo na uadilifu" alisema Bolsonaro.

Mbivu na mbichi kujulikana Oktoba 2 ambayo ni siku ya uchaguzi 

Brasilien Brasilianer protestieren in Sao Paulo für faire Präsidentschaftswahlen
Picha: Leco Viana/TheNEWS2 via ZUMA Press Wire/Zumapress/picture alliance

Pamoja na mikutano hiyo ya awali ya kampeni kutawaliwa na matamshi ya karaha, wanasiasa hao wawili waliyatumia majukwaa yao kuwaeleza wapiga kura kile watakifanya.

Lula da Silva alisema anataka kushughulikia uchumi wa nchi hiyo uwanufaishe tena watu masikini kama alivyofanya alipokuwa rais zaidi ya muongo mmoja uliopita.

Bolsonaro amewataka wafuasi wake wamwamini kwa muhula wa pili kuendeleza kazi ya kukuza uchumi licha ya mtikisiko unaoshuhudiwa hivi sasa.

Kulingana na matokeo ya kura za maoni ya umma yaliyochapishwa siku ya Jumatatu, Lula anaongoza kwa asilimia 44 dhidi ya Bolsonaro mwenye asilimia 32 lakini wapiga kura wa Brazil watafanya uamuzi rasmi katika uchaguzi wa Oktoba 2.