1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mhafidhina Bolsonaro ashinda urais wa Brazil

Daniel Gakuba
29 Oktoba 2018

Mgombea mwenye sera kali za mrengo wa kulia ameshinda duru ya pili ya urais nchini Brazil. Jair Bolsonaro ambaye kauli zake zimemfanya afananishwe na Rais Donald Trump wa Marekani amepata asilimia 55.1 ya kura zote.

https://p.dw.com/p/37IoQ
Brasilien Wahlen - Jubel bei den Bolsonaro-Anhängern
Picha: Reuters/P. Olivares

Ilikuwa shangwe na nderemo katika kambi ya mhafidhina Jair Bolsonaro, baada ya kutangazwa kwa ushindi wake dhidi ya mpinzani wake Fernando Haddad, mgombea wa kambi ya sera za mrengo wa kushoto ambaye ameambulia asilimia 44.9 ya kura katika duru ya mwisho ya kinyang'anyiro cha urais nchini Brazil.

Bolsonaro, mwanajeshi wa zamani ambaye pia amekuwa mbunge kwa miaka 27, alijinadi kama mtu aliye nje ya siasa za Brazil, akitumia lugha kali ambayo wakati mwingine ilikuwa na ujumbe unaohamasisha vurugu.

Ushindi wake unadhihirisha hasira za umma dhidi ya tabaka la wanasiasa ambao wamekuwepo madarakani, wakati rushwa ikishamiri na uchumi ukizidi kudorora. Bolsonaro aliahidi kupambana na uhalifu, na kukabiliana vilivyo na ufisadi.

Copacabana yawaka kwa fataki

Brasilien Präsidentschaftswahlen Jair Bolsonaro
Jair Bolsonaro, Rais mteule wa BrazilPicha: picture-alliance/Xinhua/L. Ming

Katika mji wa Rio de Janeiro ambao ndio mkubwa zaidi kibiashara nchini Brazil, maelfu ya mashabiki wa Bolsonaro walikuwasanyika katika ufukwe maarufu wa Cobacabana, wakiwasha fataki na kushangilia ushindi wake. Akizungumza baada ya ushindi huo, Bolsonaro aliyekuwa na Biblia mezani, amesema Wabrazil wanakaribia kujua ukweli.

''Mtafahamu ukweli, na ukweli utawafanya kuwa watu huru. Watu wa Brazil wanayo haki ya kujua ukweli, ukweli wa yanayotendeka kwenye kilele cha madaraka, katika Ikulu ya Rais.'' Amesema Bolsonaro.

Mpinzani wake, Fernando Haddad ambaye aligombea kwa niaba ya ya rais wa zamani wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva ambaye anatumikia kifungo jela, amekubali kushindwa, na kuwahimiza wafuasi wake kutotiwa hofu na utawala wa Bolsonaro.

Ushindi licha ya kauli za uchochezi

Brasilien, Fernando Haddad verliert Präsidentschaftswahl
Mgombea aliyeshindwa, Fernando HaddadPicha: picture alliance/AP Photo

Wakati wa kampeni zake, Bolsonaro aliwashitua wengi kwa maneno yake makali, ambapo ametishia kuwatokomeza wanasiasa wa mrengo wa kushoto wafuasi wa chama cha PT cha Lula da Silva, na kauli za kuwabeza wanawake, wapenzi wa jinsia moja, na makundi ya walio wachache nchini Brazil.

Rais Donald Trump wa Marekani ambaye Jair Bolsonaro alisema anamchukulia kuwa mfano, tayari amekwishatuma pongezi zake, akimtakia Bolsonaro kila la heri.

Uchaguzi huu wa Brazil umesababisha mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wananchi wa taifa hilo, ambalo ndilo kubwa zaidi katika ukanda wa Amerika Kusini.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, rtre, dw

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman