1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis awataka Wakatoliki wawasaidie masikini

25 Desemba 2021

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewataka waumini wa Kanisa hilo wawasaidie masikini na amesema wale wasiowajali masikini na watu wanaohitaji wanamkasirisha Mungu.

https://p.dw.com/p/44onb
Vatikan Christmette Papst Franziskus
Picha: Filippo Monteforte/AFP

Katika hotuba aliyoitoa wakati wa misa ya mkesha wa Krisimasi, Papa Francis pia amewasihi waumini wa Kanisa Katoliki kuthamini pia vitu vidogo katika maisha yao na kuwakumbuka wale wenye shida. Amesema watu wanapaswa kuwa na hofu ya kumkasirisha Mungu kwa kuwadharau watu masikini.

Papa pia alinukuu mstari mmoja kutoka kwenye shairi la mwandishi wa Marekani Emily Dickinson unaosema "Aliyeifikia mbingu chini yake- Atashindwa kuipata ikiwa juu yake" na akaongeza maneno yake mwenyewe: "Tusiupoteze upeo wa mbingu machoni mwetu, tumjali Yesu sasa, kwa kuwatimizia wanaohitaji, kwa maana ndani yao Yesu anajidhihirisha."

Papa Francis amesema kwamba Kanisa linapaswa kushughulikia kila aina ya umaskini na kuhubiri Injili kwa kila mtu, kwani sisi sote ni maskini, sisi sote kwa njia moja au nyingine ni wahitaji.

Kanisa la Mtakatifu Peter lililopo mjini Rome, Italia
Kanisa la Mtakatifu Peter lililopo mjini Rome, ItaliaPicha: Matteo Nardone/Pacific Press/picture alliance

Waumini wapatao 2000 na viongozi wa dini 200 walihudhuria misa iliyoongozwa na baba mtakatifu katika mkesha wa Krismasi kwenye Kanisa la Mtakatifu Peter mjini Rome na kwa wale ambao hawakufanikiwa kupata nafasi ya kuingia katika ukumbi wa kanisa hilo la mtakatifu Peter walitazama hafla hiyo kwenye skrini kubwa nje ya kanisa hilo.

Idadi ya watu waliohudhuria misa hiyo ilipunguzwa kwa thuluthi moja ya wingi watu kulinganisha na idadi ya watu walioruhusiwa katika miaka ya nyuma hatua hii ni kwa sababu ya janga la COVID-19.

Ilikuwa misa ya pili kama hii ya mkesha wa Krismasi iliyoadhimishwa wakati wa janga la corona. Mwaka jana, takriban watu 200 pekee, wengi wao wakiwa wafanyikazi wa Vatikan, walihudhuria ibada hiyo.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis wakati wa misa ya mkesha wa Krismasi 2021
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis wakati wa misa ya mkesha wa Krismasi 2021 Picha: Filippo Monteforte/AFP

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis mwenye umri wa miaka 85 pia amewashukuru wahudumu wa afya kwa kazi wanayofanya hasa wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na janga la virusi vya corona.

Kiongozi huyo wa kidini pia amesema katika msimu huu wa mwisho wa mwaka anawakumbuka watoto wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali mbalimbali duniani katika kipindi cha sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.

Vyanzo:/dpa/https://p.dw.com/p/44oji