1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis aadhimisha miaka 10 tangu kuchaguliwa

13 Machi 2023

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani papa Francis leo anaadhimisha miaka 10 tangu kuchaguliwa kwake kuwa papa.

https://p.dw.com/p/4OajT
Vatikan Papst Franziskus Rückkehr nach Italien
Picha: Tiziana Fabi/Pool via REUTERS

Papa Francis ameadhimisha mwongo mmoja ambao ni kipindi cha miaka10 kama mkuu wa kanisa katoliki duniani kwa misa pamoja na makadinali katika Kanisa la Vatican la Santa Marta, mahala ambapo ameishi tangu kuchaguliwa kwake. Papa Francis mwenye umri wa miaka 86, alishika hatamu za kuliongoza kanisa katoliki mnamo tarehe 13 mwezi Machi mwaka 2013 akimrithi Benedict 16 ambaye alijiuzulu.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa FrancisPicha: FILIPPO MONTEFORTE/AFP

Katika kutimiza kwake mwongo mmoja tangu alipochaguliwa, Papa Francis amepitia matukio kadhaa ya kihistoria na na mengine ambayo hayakuwa yamepangwa na yote hayo yamesaidia kufafanua muelekeo na vipaumbele vya papa Francis. Akizungumzia kumbukumbu za kuchaguliwa kwake, papa Francis amesimulia jinsi alivyofika Vatican akiwa na mkoba mdogo akijua kuwa baada ya zoezi la kumchagua papa mpya atarudi nyumbani lakini haikuwa hivyo.

Mnamo jioni ya tarehe13 mwezi Machi hapo mwaka 2013 alichaguliwa kuwa kiongozi wa kanisa katoliki wa 266 na kupewa jina la Papa Fracis. Na kwa mtindo tofauti kabisa na ule wa mtangulizi wake Benedict wa 16 papa Francis, alichagua kutoishi katika makazi ya Mapapa kwenye kasri la Mitume akisema kwamba yeye alihitaji kuwa karibu na watu.

Elisabetta Pique, mwandishi wa wasifu wa Papa Francis ambaye pia ni mwandishi wa Vatican wa jarida la 'La Nacion' amesema miaka 10 imekuwa ya ajabu, na kwamba anadhani watu wengi waliokuwa mbali na Kanisa walirudi Kanisani kwa sababu papa Francis ni mtu anayeweza kuzungumza kwa njia rahisi sana na kila mtu.

Soma: Papa Francis akanusha kuwa anapanga kujiuzulu hivi karibuni

Papa Francis anaadhimisha mwongo mmoja tangu kuchaguliwa kuliongoza kanisa katoliki duniani akikabiliwa na upinzani ndani ya kanisa katoliki ambapo mara kadhaa wahafidhina ndani ya kanisa hilo wamekuwa wakimtaka ajiuzulu ingawa kwa sasa wako kwenye njia panda wakitafuta mwelekeo mpya baada ya vifo vya viongozi wao wakuu wawili. Kwa upande wake papa Francis amesema atakuwa tayari kuondoka madarakani iwapo matatizo ya kiafya yatamzuia kuendesha Kanisa katoliki lenye waumini bilioni 1.38na si vinginevyo.

Vyanzo:RTRE7APA