1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Pande zinazohasimiana Sudan zaanza mazungumzo ya amani

12 Julai 2024

Pande zinazohasimiana katika mzozo nchini Sudan zimewasili mjini Geneva kufuatia mwaliko wa Umoja wa Mataifa ili kujadiliana kuhusu kuwalinda raia ikiwa kutafikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/4iCCK
Mzozo wa Sudan | Hali ya kiutu
Changamoto kubwa iliyosababishwa na mzozo kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF ni wakimbizi wa ndani waliokimbia mapigano, kama kwenye picha hiiPicha: Omer Erdem/Anadolu/picture alliance

Maafisa wa Umoja wa Mataifa hata hivyo wamesema jana Alhamisi kwamba ni upande mmoja tu ndio ulishiriki katika siku ya kwanza ya mazungumzo.

Msemaji wa umoja huo, Stephane Dujarric amesema wawakilishi waandamizi kutoka jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF walikubali kukutana kwa nyakati tofauti na mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ramtane Lamamra. 

Dujarric hakutaja wawakilishi walioshiriki mazungumzo, lakini alisema Lamamra na timu yake walikutana na wawakilishi hao na kuzikaribisha pande zote kuendelea na mazungumzo hii leo.