1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Pande hasimu zaendelea kupigana nchini Sudan

Admin.WagnerD13 Mei 2023

Ndege za kivita zimefanya hujuma kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum huku mapigano ya mitaani yakiendelea bila dalili ya kupatikana mkataba wa kumaliza vita.

https://p.dw.com/p/4RITd
Mapigano mjini Khartoum, Sudan
Mapigano mjini Khartoum, SudanPicha: Mohamed Nureldin/REUTERS

Hujuma hizo zimeripotiwa ikiwa ni siku moja tangu pande hasimu kukubaliana kanuni za kuwalinda raia na kuruhusu usambazwaji wa misaada ya kiutu bila vizingiti. Makubaliano hayo yaliyotiwa sana siku ya Alhamisi mjini Jeddah, hayakujumuisha lakini mkataba wa usitishaji mapigano.

Karibu mwezi mmoja baada ya kuzuka mapigano nchini Sudan ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 750 na kuwalazimisha maelfu wengine kuzikimbia nyumba zao, bado hakuna ishara za mzozo huo kufikia mwisho.

Licha ya makubaliano ya mjini Jeddah, kunakofanyika mazungumzo ya kujaribu kumaliza vita, vikosi vya pande hasimu vilishambuliana siku ya Ijumaa katikati ya viunga vya mji mkuu, ambao ni makaazi ya zaidi ya watu milioni 5.

Shuhuda mmoja ameliambia Shirika la Habari la AFP alisikia mingurumo ya ndege za kivita na milipuko ya makombora.

Huko magharibi mwa jimbo la Darfur, eneo amablo pia limeshuhudia mapigano makali, watu walitafuta maeneo ya kujificha kutokana na mashambulizi makali ya makombora na risasi. Hayo yameelezwa na mashuhuda waliozungumza na AFP.

Matumaini ya kupatikana mkataba wa amani bado ni madogo 

Abdul Fattah Al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo
Abdul Fattah Al-Burhan na Mohamed Hamdan DagaloPicha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Wawakilishi wa majenerali wawili wanaowania madaraka ambao ni mkuu wa jeshi na kiongozi wa taifa, Abdel Fattah al-Burhan na mwenzake anayeongoza kikosi cha wanamgambo wenye nguvu cha RSF, Mohamed Hamdan Daglo, walikubaliana mjini Jeddah kuhakikisha misingi ya kuwalinda raia inazingatiwa.

Makubaliano hayo yanajumuisha pia dhamira ya kila upande ya kuruhusu kusambazwa msaada wa kiutu kwa wanaohitaji na yanatoa mwito wa kurejeshwa huduma muhimu za kijamii kama maji na umeme.

Marekani na Saudi Arabia zinazoongoza juhudi za kidiplomasia za kuutatua mzozo huo, zimesema mashauriano bado yanaendelea ili kufikiwa mkataba wa kusitisha mapigano kwa siku 10 na kisha kufungua njia ya kutafuta makubaliano ya kukomesha kabisa mapigano.

Hata hivyo wanadiplomasia wa Marekani wamekuwa wawazi juu ya vizingiti vilivyopo katika mazungumzo ya mjini Jeddah yalimaliza wiki nzima.

Idadi ya waliokimbia mapigano yapindukia watu 200,000

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Sudan Volker Perthes aliyakaribisha makubaliano ya kuruhusu usambazwaji msaada wa kiutu yaliyofikiwa baina ya pande hasimu.

Raia wa Sudan wakitafuta hifadhi
Idadi ya watu waliokimbia Sudan imefikia laki 2Picha: Amanuel Sileshi/AFP

Ameyataja kuwa "hatua ya manufaa" huku akitoa rai kwa pande hizo kuendelea na majadiliano bila kuchoka. Siku ya Ijumaa kulikuwa na tetesi kwamba mkataba wa kusitisha mapigano ungepatikana jioni au leo Jumamosi.

Tangu kuanza kwa mapigano mnamo April 15, karibu watu 200,000 wameikimbia Sudan. Makadirio hayo yametolewa na Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa.

Pia inaarifiwa kwamba wafanyakazi 18 wa huduma za msaada wa kibinadamu wameuwawa, hali iliyoyalazimisha mashirika mengi ya kimataifa kusitisha shughuli zake nchini Sudan.

Vilevile kuna ripoti za wizi wa chakula cha msaada nchini humo. Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada wa Chakula, WFP, limesema chakula cha msaada kilichoporwa au kuunzwa kimagendo kina thamani ya mamilioni ya dola.