1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila awasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Ruto

Babu Abdalla Thelma Mwadzaya
22 Agosti 2022

Wanasiasa wa Azimio la Umoja One Kenya hii leo wamewasilisha ombi la kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa tarehe 9 mwezi Agosti.

https://p.dw.com/p/4Fskm
Kenia | Raila Odinga
Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kwa mara ya kwanza tangu kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais, mwenyekiti wa tume amekutana ana kwa ana na makamishna wanne waliotofautiana na matokeo hayo.

Wakiwasili kwenye mahakama ya juu na lori zima la maboksi yaliyosheheni hati za ushahidi, mawakili wa Azimio la Umoja One Kenya walikuwa wamejihami.

Kikosi hicho kilisindikizwa na Raila Odinga anayewania urais, mgombea mwenza wake Martha Karua, vigogo wa siasa pamoja na mashabiki na wafuasi wao waliojaa kwenye eneo hilo la mahakama ya juu.

Mawakili hao walipewa muda hadi saa nane mchana kuwasilisha malalamishi hayo mbele ya mahakama. Hata hivyo walishawasilisha kielektroniki kabla ya kufika mahakamani.

Soma pia: Ujumbe wa Marekani wataka Kenyatta kukabidhi madaraka kwa amani

Dhamira ya kufika mahakamani ni kuonyesha muda haswa ilipozipokea hati hizo.Azimio sasa inalazimika kuwasilisha pingamizi hizo kwa watakaowajibu ambayo ni tume ya uchaguzi IEBC na wengine wa kambi ya rais mteule William Ruto.

Azimio sasa ina muda wa saa 24 kuwasilisha malalamiko rasmi kwa kambi ya rais mteule William Ruto aliyetangazwa mshindi na tume ya uchaguzi pamoja na wengine.Katika muda wa siku 14 kesi itasikilizwa na mahakama ya juu.

Kabla ya kufika mahakamani, kikosi cha Azimio tayari kiliwasilisha pingamizi kwa njia ya elektroniki ili kuokoa muda kwani leo ndiyo iliyokuwa siku ya mwisho kulingana na ratiba na katiba.

Kwa mujibu wa Azimio, wanachokipinga ni kuwa idadi ya waliosajiliwa na waliopiga kura haiambatani, kadhalika idadi ya waliojitokeza kwenye ngome za wapinzani wao wa Kenya Kwanza pia inatiliwa shaka.

Soma pia: Ruto: Kutoka mpwaguzi hadi rais aliechaguliwa Kenya

Akiwa kwenye jumba la mikutano la KICC Raila Odinga wa Azimio alisema kuwa muda umewadia kufanya kwa vitendo ili kuwamaliza wezi wa demokrasia wanaoirejesha nchi nyuma na kuihujumu. "Muda mfupi uliopita tumefanikiwa kuwasilisha pingamizi letu la uchaguzi wa rais katika mahakama ya juu ya Kenya. Hatua tuliyoichukuwa inakwenda sawa sawa na katiba yetu kuhusiana na suala la kuitatua mivutano ya uchaguzi. Inadhihirisha namna tulivyo na imani na katiba, utawala wa sheria na utatuzi wa amani wa mivutano ikiwemo ile mikubwa  kama uchaguzi wa rais. tumeshangazwa kuona wakati tunajiandaa kwenda mahakamani wengine walijaribu kutuzuia."

Wanasiasa hao pia wanadai kuwa vifaa vya kuwatambua wapiga kura siku ya uchaguzi vilikuwa na dosari. Jopo la majaji 7 litasikiliza kesi hiyo itakayowaleta pamoja wawakilishi wa Azimio, rais mteule William Ruto na tume ya uchaguzi IEBC. Tayari IEBC imetangaza kuwa maeneo yaliyoahirisha uchaguzi yataweza kutimiza haki yao ya kikatiba tarehe 29 mwezi huu. Wafula Chebukati ni mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, IEBC.

Mchakato huo ni kwa ajili ya ubunge wa Rongai, Kitui rural, Kacheliba na Pokot Kusini pamoja na ugavana wa Mombasa na Kakamega.

Itakumbukwa kuwa makamishna wanne wa Tume ya uchaguzi walitofautiana na hesabu iliyotangazwa na mwenyekiti na kushikilia kuwa hawakupewa nafasi kuuliza maswali. 

Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi itakamilika mwanzoni mwa Septemba kulingana na ratba ya katiba.