1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New York. Mkutano wa kuangalia upya kuenea kwa silaha za kinuklia wamalizika bila mafanikio muhimu.

28 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CF9U

Mkuu wa kitengo kinachoangalia masuala ya kinuklia katika umoja wa mataifa Mohammed el Baradei amesema kuwa kushindwa kwa mkutano wa umoja wa mataifa wa kuzuwia kuenea kwa silaha za kinuklia, kuidhinisha hatua mpya za kupambana na kuenea kwa silaha hizo kunatia wasi wasi na kwamba viongozi wa jumuiya ya kimataifa ni lazima sasa walenge katika suala hilo.

Wakati mkutano huo unaoangalia upya mkataba wa mwaka 1970 wa kuzuwia kuenea kwa silaha za kinuklia ukimalizika katika makao makuu ya umoja wa mataifa mjini New York , amesema kuwa baada ya mwezi mzima , mkutano huo umemalizikia pale ulipoanzia , ukiwa na mfumo wenye matundu kadha na sio mpango kamili wa kuyaziba.

Mataifa 150 yaliyohudhuria, yameshindwa kukubaliana katika hatua yoyote mpya kuzuwia ueneaji wa silaha hizo, licha ya hali ya wasi wasi inayozidi kukua juu ya kuenea kwa silaha hizo.

Kuangaliwa upya kwa mkataba wa mwaka 1970 kulichangiwa na mijadala inayogawa hasa kuhusu Korea ya kaskazini, haja ya Iran kuendelea na kurutubisha madini ya Uranium, madai ya kuwapo kwa silaha za kinuklia nchini Israel na mipango ya Marekani ya silaha mpya na za kisasa za kinuklia, pamoja na mvutano juu ya utaratibu wa kuendesha mambo.