1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Usalama mjini Munich, Ukraine yasema yataka amani

Zainab Aziz Mhariri: Jacob Safari
19 Februari 2022

Viongozi wa nchi za Magharibi wameionya Urusi juu ya kuihamisha mipaka ya taifa jingine kwa nguvu na kwamba hatua kama hiyo itakabiliwa na majibu makali yatakayoiathiri Urusi kiuchumi .

https://p.dw.com/p/47HqB
Münchner Sicherheitskonferenz MSC
Picha: Andrew Harnik/REUTERS

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amesema kwenye mkutano wa masuala ya usalama wa mjini Munich kwamba Marekani itazidi kuwaimarisha wanachama wa NATO wa upande wa Ulaya mashariki ikiwa ni nyongeza itakayoandamana na hatua za vikwazo dhidi ya Urusi ili kuizuia nchi hiyo kufanya uvamizi wowote wa kijeshi dhidi ya Ukraine.

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris
Makamu wa Rais wa Marekani Kamala HarrisPicha: Tobias Hase/dpa/picture alliance

Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris alikutana na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kabla ya kuhutubia mkutano wa usalama wa mjini Munich. Harris alisema ``huu wakati madhubuti katika historia" na akamwambia rais wa Ukraine kwamba tishio lolote kwa nchi ya Ukraine Marekani inalichukulia kwa uzito mkubwa. Naye rais wa Ukraine alimjibu: ``Tunaelewa wazi kinachoendelea. Ukraine ni ardhi yetu na tuchotafuta ni Amani'.

Zelenskiy, ambaye alizungumza kwa kifupi, pia alisema Ukraine inatafuta msaada maalum kutoka Marekani kwa ajili ya jeshi lake.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Irina Yakovleva/TASS/dpa/picture alliance

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema Urusi itabanwa katika kuyafikia masoko ya fedha na bidhaa za kielektroniki chini ya vikwazo vya nchi za Magharibi vinavyoandaliwa iwapo Urusi itaishambulia Ukraine.

Soma:Guterres: Kitisho kwa usalama wa dunia kikubwa zaidi sasa

Rais wa Marekani Joe Biden alisema siku ya Ijumaa kuwa ameshawishika kwamba rais wa Urusi Vladimir Putin ameamua kuivamia nchi hiyo jirani yake.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kwenye mkutano huo wa usalama unaofanyika kila mwaka mjini Munich kwamba alipokutana na rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Jumanne, alimweleza wazi kuwa ukiukaji wowote wa mipaka ya Ukraine utaitumbukiza Urusi kwenye gharama kubwa katika Nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijiografia. Wakati huo huo, Scholz amesisitiza kwamba njia zote za kidiplomasia zitumike pakubwa.

Majaribio ya makombora ya Urusi ya 19.02.2022
Majaribio ya makombora ya Urusi ya 19.02.2022Picha: Russian Defense Ministry/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo Urusi imefanyia majaribio makombora yenye uwezo wa nyuklia siku ya Jumamosi katika zoezi kubwa la kijeshi lililosimamiwa na Rais Vladimir Putin huku Marekani ikionya tena kwamba inaamini Moscow inapanga kuivamia Ukraine katika siku chache zijazo.

Soma:Urusi yasema luteka za nyuklia ni salama

Urusi imekanusha na inasisitiza kuwa haina mpango wa kuishambulia nchi jirani yake, licha ya Ukraine kuikasirisha Urusi kwa kutafuta uhusiano wa karibu na NATO na Umoja wa Ulaya.

Vyanzo: RTRE/DPA/AP/AFP