1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi sita za Afrika kuanza kutengeneza chanjo ya COVID-19.

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
18 Februari 2022

Nchi za kwanza sita za Afrika zitapokea teknolojia ya kutengeneza chanjo ya mRNA dhidi ya COVID-19. Hayo yametangazwa mjini Brussels kwenye mkutano wa kilele kati ya viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika.

https://p.dw.com/p/47FKQ
Belgien Brüssel | EU-Afrika-Gipfel | Olaf Scholz
Picha: Yves Herman/AFP/Getty Images

Nchi hizo sita ambazo ni Misri, Kenya, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia zitapokea teknolojia hiyo kutoka kwenye Kituo cha kimataifa cha kutengeneza chanjo za mRNA cha Shirika la Afya Duniani WHO kilichopo nchini Afrika Kusini, lengo likiwa ni kuziwezesha nchi hizo kuanza kutengeneza chanjo haraka iwezekanavyo.

Rais wa Senegal Macky Sall ambaye pia ni rais wa sasa wa Umoja wa Afrika akizungumza na waandishi wa habari mjini Brussels 17.02.2022.
Rais wa Senegal Macky Sall ambaye pia ni rais wa sasa wa Umoja wa Afrika akizungumza na waandishi wa habari mjini Brussels 17.02.2022.Picha: John Thys, Pool Photo/AP/picture alliance

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameusifu mpango huo na amesema unaleta matumaini kwa bara la Afrika. Mwenzake wa Senegal Macky Sall amesema lengo la bara hilo ni kuweza kutoa chanjo kwa asilimia 60 ya watu wa bara la Afrika na chanjo hizo pia ziwe zimetengenezwa barani humo.

Soma:Viongozi wa Ulaya na Afrika wakusanyika Brussels

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya na wenzao kutoka nchi za Afrika pamoja na baadhi ya mashirika ya kimataifa walikutana Ijumaa katika hafla ya mkutano wa kilele wa 6 mjini Brussels. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, pamoja na Rais wa Halmshauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen waliungana na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kutangaza mafanikio ya mradi huo ulioanzishwa na WHO wa kutengeneza chanjo za COVID-19 ndani ya bara la Afrika. Ramaphosa amesema tamko la leo maana yake ni kuheshimiana na kutambua kwamba nchi za Afrika zinaweza kuchangia katika uwekezaji vitega uchumi kwa ajili ya bara hilo.

Akipongeza mafanikio hayo rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisisitiza kuwa mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kuanzisha na kuimarisha soko la chanjo barani Afrika. Amesema haikubaliki kuwa Afrika ibaki nyuma ya foleni kila mara kuhusiana na upatikanaji wa dawa.

Kushoto: Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Katikati: Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel Kulia: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Kushoto: Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Katikati: Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel Kulia: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.Picha: Olivier Hoslet/AFP/Getty Images

Ramaphosa pia amesisitiza wito wake juu ya kuondolewa hati miliki za chanjo za corona ambazo anaamini wazalishaji zaidi wangeruhusiwa kutengeneza dozi hizo. Umoja wa Ulaya unaendelea kupinga na badala yake unataka makubaliano kati ya nchi husika na kampuni ili kuhamisha tekinolojia na ujuzi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus ameuambia mkutano wa mjini Brussels kwamba ingawa zaidi ya dozi bilioni 10 za chanjo za COVID-19 zimetolewa duniani kote, mabilioni ya watu bado hawajapata chanjo. Ameendelea kutoa wito wa upatikanaji sawa wa chanjo ili kukabiliana na janga la corona.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus.Picha: Jaber Abdulkhaleg /AA/picture alliance

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Afrika wanakutana kwenye mkutano wa kilele wa siku mbili ulioanza Alhamisi lengo kuu likiwa ni kuanzisha upya uhusiano kwa kutoa ahadi za uwekezaji mkubwa ili kukabiliana na ushindani kutoka China na Urusi.

Mahusiano kati ya mabara hayo jirani yametatizwa na msururu wa matatizo. Pande hizo mbili zinavutana juu ya chanjo ya COVID-19 huku Ulaya ikikhofia kuongezeka kwa ushawishi wa China na Urusi katika bara la Afrika ambalo ni tajiri kwa rasilimali lakini lenye nguvu ndogo za kiuchumi duniani. Viongozi hao zaidi ya 40 wa Afrika na Ulaya wanaokutana mjini Brussels wanatarajiwa kukamilisha mkutano huo wa kilele hii leo. 

Vyanzo: AP/RTRE