1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Kigeni zaondosha raia wake Sudan

24 Aprili 2023

Hali ya wasiwasi na vita imesababisha mataifa mbali mbali ya kigeni kuharakisha juhudi za kuondosha raia wake nchini Sudan kupitia njia za anga,bahari na barabara

https://p.dw.com/p/4QTzF
Soldaten der Bundeswehr in Jordanien
Picha: Weyland/Bundeswehr/dpa/picture alliance

Vita nchini Sudan vimesababisha mataifa ya kigeni kuanzisha operesheni za kuondowa raia wao. Juhudi za uokoaji raia wa kigeni au wafanyakazi wa ofisi za kibalozi zinafanyika kwa njia ya barabara, ndege na bahari. Ujerumani ni miongoni mwa nchi ambazo zimetumia ndege kuwaondowa raia wake na wa nchi nyingine za Ulaya.

Uwanja mkubwa wa ndege katika mji mkuu, Khartoum ni eneo ambalo hasa ndiko yanakoshuhudiwa mapigano makali na unadhibitiwa na kikosi maalum cha wanamgambo wa Rapid Surpport Forces, RSF wanaopambana na jeshi la serikali ya Sudan.

Hii leo Jumatatu mataifa ya Umoja wa Ulaya, China na nchi nyingine za ulimwengu zimeonekana kutumia fursa ya utulivu kiasi kuharakisha juhudi za kuwaondowa maelfu ya raia wao kutoka mji huo wa Khartoum. Mataifa mbalimbali yamewaondowa raia wao kwa ndege, magari na kupitia njia ya bahari ya sham kutokea bandari ya Sudan.

Videostill - Saudi Arabischer Fernsehsender - Evakurierung saudischer Bewohner
Picha: AL-IKHBARIYA TV/AFP

Jana Jumapili jeshi la Marekani lilipeleka helikopta aina ya Chinook kuwaondosha wafanyakazi wa ubalozi wake kutoka Khartoum ambapo zaidi ya wanajeshi 100 wa Marekani walishiriki zoezi hilo la kuwaondowa chini ya watu 100 kwa kipindi cha chini ya saa moja. Pia maafisa wa Marekani wametoa tahadhari kwamba hakuna uwezekano wa kufanyika operesheni pana ya kuwaondoa raia wa Marekani katika kipindi cha siku kadhaa zijazo.Majeshi ya Ujerumani yaendelea na operesheni ya kuwahamisha watu ktoka Sudan inayokabiliwa na mapigano

Umoja wa Ulaya nao jana pia ulisema ziopo juhudi za kushirikiana za kuwaondosha raia wa jumuioya hiyo walioko Sudan ikiwa ni pamoja na ujumbe wa Umoja huo. Nchi saba za Umoja wa Ulaya zina balozi zake ndani ya Sudan.

Na kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi Wopke Hoekstra raia wake wachache wameshaondolewa na ndege ya Ufaransa huku kundi jingine likisafirishwa kwa njia ya barabara kutoka Khartoum kupitia msafara wa magari ya Umoja wa Mataifa. Ufaransa ilipeleka ndehe mbili zilizotuwa Djibouti Jumapili na kuwabeba jumla ya watu 200 raia wa mataifa mbali mbali. Ufaransa na Ujerumani hii leo zimesema tayari zimeshaondowa kiasi watu 700 bila ya kutaja ni raia wa nchi zipi.

Soldaten der Bundeswehr in Jordanien
Picha: Neumann/Bundeswehr/dpa/picture alliance

 Ndege ya jeshi la anga la Ujerumani ikiwa imewabeba watu kutoka Khartoum ilituwa mjini Berlin asubuhi ya leo. Kwa ujumla katika Umoja wa Ulaya, kwa mujibu wa mkuu wa sera za nje wa Umoja huo, mjini Brussels, Joseph Borrell zaidi ya raia 1,000 wa nchi za umoja huo wameondolewa nchini Sudan katika kipindi cha mwishoni mwa Juma. Borrell amesema ilikuwa ni operesheni ngumu japo imefanikiwa pia alizungumza na makamanda wawili mahasimu Abdel Fattah al Burhani na Mohammed Hamdan Dagalo na kuwataka wasitisha vita mara moja.

''Jumuiya ya Kimataifa kwa pamoja wanazishinikiza pande zote mbili zisitishe vita. Ndio nimekuwa nikizungumza na nchi zote jirani na marafiki na hata majenerali wawili walioko vitani na ujumbe wa jumuiya ya kimataifa ni huo huo,Vita visitishwe.''Burhan amani ya Sudan itapatikana kwa mazungumzo

Sudan Konflikt l Satellitenfoto von Planet Labs PBC zeigt Feuer am internationalen Flughafen von Khartum
Picha: Labs PBC via AP/picture alliance

Hali bado sio shwari nchini Sudan na nje ya mji mkuu,kwa mujibu wa taarifa mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo Jumatatu, watu wameripotiwa kuyakimbia mapigano katika majimbo mengine chungunzima ikiwemo majimbo matatu ya Darfur, Blue Nile katika eneo la mpaka na Ethiopia na Sudan Kusini na Jimbo la Kordofan Kaskazini lililoko Kusini Magharibi mwa Khartoum.

Vita vilivyozuka ghafla kati ya jeshi rasmi la Sudan na wanamgambo wa RSF mnamo Aprili 15 vimesababisha mgogoro wa kibidamu ndani ya nchi hiyo na mpaka sasa watu 420 wameuwawa.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW