1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Nchi za kanda ya Balkani zawania kujiunga na Umoja wa Ulaya

Angela Mdungu
4 Oktoba 2023

Mataifa mbalimbali kuanzia Ukraine hadi nchi za kanda ya Balkani magharibi ziko kwenye harakati za kufanya mabadiliko ili zikidhi vigezo vya kujiunga na Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/4X6uw
EU-Ungarn | Sitz der EU-Kommission in Brüssel
Picha: Yves Herman/REUTERS

Makubaliano ya pamoja yalifanyika mjini Brussels tangu mwezi Februari mwaka uliopita kuwa Umoja wa Ulaya unahitaji kukua.

Wakati fulani, nchi wanachama wa Umoja huo hazikuwa zikikubaliana na suala la kuongeza wanachama lakini hivi sasa wanaafikiana kuwa ni muda muafaka wa kuzikaribisha nchi kama Ukraine, Moldova na zile za Balkani magharibi kwenye Umoja huo.

Mabadiliko haya yalichochewa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Kabla ya hapo mipango legevu ya kuupanua Umoja wa Ulaya ilikuwa wazo lililopigwa dana dana kutoka utawala mmoja hadi mwingine wakati mataifa yaliyoonesha nia ya kujiunga kama vile Macedonia ya Kaskazini inayowania nafasi hiyo tangu mwaka 2005, yakikumbana na mlolongo wa mabadiliko ya kisiasa na mahakama ili yafuzu kujiunga.

Soma pia:Viongozi wa EU na mataifa ya Balkan wakutana nchini Albania 

Orodha rasmi ya mataifa yanayoomba kujiunga na Umoja wa Ulaya ni pamoja na Ukraine, Moldova, Albania, Montenegro, Bosnia na Herzegovina, Macedonia kaskazini, Serbia na Uturuki. Georgia na Kosovo nazo zinatajwa kuwa na uwezekano wa kutaka kujiunga.

Pamoja na Umoja wa Ulaya kuwa na wanachama 27, wakati mwingine umoja huo unapata tabu kuchukua hatua.

Hatua za sera za kigeni kama vile kuiwekea vikwazo Urusi zinahitaji kuungwa mkono kwa sauti moja, hii ikimaanisha kuwa wakati mwingine mazungumzo yanaweza kuchukua miezi kadhaa wakati nchi wanachama zikijadili kwa kina ni bidhaa zipi za kuzipiga marufuku na ni mali za nani zinapaswa kuzuiliwa.

Mabadiliko katika maeneo mengine ya sera kama vile uhamiaji na maombi ya hifadhi yanahitaji kuungwa mkono  kutoka kwa mataifa makubwa yaliyofuzu ambayo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya hii ikimaanisha, walau nchi 15 ambazo zinawakilisha asilimia 65 ya wakaazi katika Umoja huo.

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Tayyip ErdoganPicha: AFP

Katika mfumo wa sasa, Ukraine yenye zaidi ya raia milioni 40 inaweza kuwa moja ya nchi zenye nguvu zaidi ndani ya Umoja wa Ulaya iwapo itajiunga. Kwa upande mwingine, kila taifa dogo  la Balkan Magharibi kama vile Montenegro yenye takribani watu 620,000 au Albania yenye wakaazi wasiopungua milioni 2.7 yanaweza kupaza sauti zao katika mchanganyiko huo.

Mtaalamu wa ngazi ya juu wa masuala ya kisera katika kituo cha Jacques Delors cha Berlin, Thu Nguyen anasema kadri wanachama wanavyozidi kuongezeka, ndivyo hatari inavyozidi ya kuwa na washiriki wengi zaidi wenye kura ya veto inayozuia maamuzi. 

Suala hilo linaweza kuwa na ugumu zaidi kwa miito ya kisiasa kama vile kuzuwia ufadhili wa Umoja wa Ulaya kwa nchi zinazotuhumiwa kukiuka viwango fulani vya utawala wa sheria.

Soma pia: Maoni: Uwanachama wa Umoja wa Ulaya sasa ubadilike

Pia kuna suala kuhusu mgawanyo wa fedha za Umoja wa Ulaya  katika mataifa yenye tofauti kubwa za kiuchumi.

Wanachama wengi wanaoomba kujiunga wana pato dogo la taifa kuliko nchi masikini zaidi mwanachama kwa sasa ambayo ni Bulgaria.

Wakati theluthi ya bajeti ya Umoja huo inapelekwa kwenye ruzuku za kilimo, uwepo wa Ukraine ambayo ina shughuli nyingi za kilimo itabadilisha pakubwa mgawanyo wa sasa 

Lakini pia kuna maswali madogo madogo ya kila aina kuhusu namna Umoja wa Ulaya ulio mkubwa zaidi utakavyofanya kazi. Kwa mfano, ni wabunge wangapi wataingia kwenye bunge la umoja huo na kutakuwa na lugha nyingine ngapi rasmi.