1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU na mataifa ya Balkan wakutana nchini Albania

6 Desemba 2022

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na wenzao wa nchi za Balkan Magharibi wamekutana mjini Tirana nchini Albania kujadili kuimarisha mahusiano wakati uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ukiongeza shinikizo la kutanuliwa muungano huo.

https://p.dw.com/p/4KYcP
Albanien EU-Gipfel Tirana
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Lengo la mkutano huo ni kulihakikishia eneo hilo kuhusu mustakabali wao katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya katika wakati ambapo ushawishi wa Urusi na China unaongezeka. Akiwa kwenye mkutano huo, Charles Michel, rais wa baraza la Umoja wa Ulaya akizungumza mwanzoni mwa mkutano huo amesema mustakabali wa nchi hizo uko ndani ya Umoja wa Ulaya.

"Nimejiridhisha vya kutosha kwamba mustakabali wa watoto wetu utakuwa salama na wenye maendeleo tukiwa na nchi za Balkan Magharibi ndani ya Umoja wa Ulaya na tunafanya kazi kwa bidii kupiga hatua. Leo kwa mfano, tutatia saini makubaliano kuhusu mawasiliano ya simu za mkononi, hii ni hatua madhubuti tulioijadili tukiwa Brdo, Slovenia zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Ni hatua muhimu kwa biashara, wananchi wetu, na utalii inayotuelekeza mahala sahihi'' amekaririkiwa Bw. Michel.

Nchi za eneo la Balkan kwa miaka zinasubiri kuingizwa kwenye Umoja wa Ulaya na mara kwa mara zimekuwa zikizungumzia kuchoshwa kwao na mchakato mrefu na wenye masharti mengi.

Mkutano wa kilele unaofanyika Tirana unawajumuisha viongozi wa Albania, Bosnia ,Montenegro, Kosovo, Macedonia Kaskazini na Serbia.