1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za G20 kuhakikisha ugavi wa haki wa chanjo ya corona

Zainab Aziz Mhariri: Lilian Mtono
22 Novemba 2020

Katika tamko lao la pamoja viongozi wa nchi za G20 wanatarajiwa kutoa ahadi ya kuhakikisha haki inazingatiwa katika ugavi wa chanjo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3lg8b
Virtueller G20-Gipfel | Russland
Picha: Alexei Nikolsky/dpa/picture alliance

Viongozi hao pia wameungana katika msimamo wa kuunga mkono biashara ya kuyashirikisha mataifa yote duniani na kuunga mkono juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Hata hivyo tamko hilo halizingatii kwa undani masuala yaliyotawala kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa G20 wa mjini Riadh,Saudi Arabia uliofanyika kwa njia ya video.

 Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (Virtueller G20-Gipfel | Deutschlan)
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Guido Bergmann/picture alliance

Soma zaidi:IMF na kundi la G-20 zatoa nafuu kwa mataifa masikini

Mkutano huo wa siku mbili kuanzia hapo jana umefanyika katika muktadha wa juhudi kubwa kwa lengo la kugawa chanjo ya COVID -19 kwa kiwango kikubwa baada ya kupatikana mafanikio ya majaribio ya chanjo kadhaa na wakati ambapo viongozi wa Umoja wa Ulaya na wa nchi nyingine wanatoa wito wa kuchangisha fedha ili kuziba pengo la dola bilioni 45.   

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema maradhi ya Covid -19 ni mtihani kwa nchi za G20 na kwa hivyo njia ya ufanisi ya kupambana na janga hilo ni ushirikiano wa nchi zote duniani. Watu zaidi ya milioni 56 wameambukizwa virusi vya corona na wengine wapatao milioni 1.3 wameshakufa duniani kote.

Soma zaidi:Mkutano wa G20 kutawaliwa na siasa za ndani

Hata hivyo viongozi wa nchi za G20 wamebanwa na shikiniko la kujaribu kuepusha nchi masikini kushindwa kulipa madeni yao. Kwa sasa nchi tajiri zimerefusha muda wa kusimamisha ulipaji wa riba hadi mwezi Juni mwaka ujao, chini ya mpango unaoitwa DSSI lakini katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anataka muda huo urefushwe hadi mwishoni mwa mwaka ujao. Hata hivyo hakikisho hilo  halijatolewa. Mawaziri wa fedha watalitafakari pendekezo hilo mwaka ujao kwenye mkutano wa shirika la fedha la kimataifa IMF.

Kuhusu biashara, nchi tajiri duniani pia zimesisitiza haja ya kuunga mkono mfumo wa ushirikiano wa nchi zote.Viongozi wa nchi hizo tajiri wamesema wanalenga shabaha ya kuleta biashara huru na ya haki kwa wote bila ya kuzibagua nchi nyingine, wamesema wanataka uwazi, mazingira ya biashara imara na ya kuwekeza vitega uchumi, ili kuyaweka masoko wazi.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ( EU-Kommissions Präsidentin von der Leyen telefonier)
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Thierry Monasse/dpa/picture alliance

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema anatumai kuwa Marekani itafuata njia ya ushirikiano wa mataifa yote chini ya utawala ujao wa Joe Biden na pia ameelezea matumaini ya mwafaka kutoka Marekani juu ya juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuirejesha Marekani kwenye mkataba wa Paris juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Chanzo:/ AFP/DPA